Wednesday 21 March 2012


UNAPOFIKIA KUJUTIA ASILI YAKO






Kama kuna utumwa na ufukara wa mawazo, basi ni pamoja na panapokuwepo na hisia hii na kufikia kujuta kuwa wa asili fulani.
Hutokea mtu akajuta kimoyomoyo na baadae kujikuta akitamka bayana kuwa anajuta kuwa mwanamume, au anajuta kuwa mhehe, ama anajuta kuwa Mtanzania n.k. Mtu anajikuta anajuta kwa sanabu zake binafsi kiasi cha kuikashfu jamii yake nzima. Mara nyingi hata kile kinachosababisha akajuta huwa kwa ukweli wa mambo hakina msingi. Kujuta wewe kuwa Mtanzania kwa uwingi wake ni kuamini kuwa watanzania wana kasoro.
Unakuta mtu anajuta kuzaliwa mtanzania kwa sababu tu hana kazi au ajira. Anakuwa anawaza kuwa pengine angelizaliwa marekani angelikuwa hana tatizo hilo. Mwingine hujuta kuwa mwanamume kutokana na kuelemewa na majukumu, anawaza kuwa pengine angelizaliwa mwanamke angeliolewa na kuwa tegemezi; lakini hajakaa akafuatilia kuona ni mazito mangapi yanayowakabili wanawake.
Wazo na hisia hizo kidogo zina nafuu lakini inapopindukia na kumkuta mtu anatamka waziwazi tena kwa kujiamini kabisa kuwa ni heri angelizaliwa mbwa uingereza kuliko kuzaliwa mtu Tanzania hapo ndipo kazi inapokuwa kubwa ya ushauri nasaha. Inabidi ufuatilie kwa undani sana ili kujua sababu hasa za mtu huyu kufikia kuona bora awe bobi ugenini kuliko kuwa mwenyeji katika nchi yake.
Waswahili wanasema mtu unapokuwa fukara wa mawazo unakuwa unatisha kushinda hata mwendawazimu. Mwanafunzi wa chuo kuona heri angelizaliwa mbwa Ulaya kutokana na kucheleweshewa mkopo, mwanamume kuona heri angelizaliwa mwanamke kutokana na kushindwa kuihudumia familia yake, mwanamke kuona heri angelizaliwa mwanamume kutokana na kunyanyasika kimapenzi n.k. kukurejesha katika mawazo ya kawaida kunahitajika kazi ya ziada.
Mawazo ya aina hii ni matokeo ya watu kujifungia vioo na kujibinafshia matatizo. Kuona wao ndio wenye matatizo makubwa kushinda watu wote. Kutarajia mazuri tu katika maisha yao. Kujiona wao wako kamili kimawazo na kifikra kiasi cha kutohitaji kujifunza au kupata ushauri kutoka kwa wengine. Daima hatma ya watu hawa kama si kunywa sumu, au kujinyonga huihujumu jamii kwa itikadi zao, vurugu zao, na visasi vyao. Hawa ndio kama wanavyodai wao kuwa ni mbwa wa kizungu ambao wanalazimika kujifanya watu katika jamii yetu. Watu hawa daima huwa hawaishiwi na hoja; huwa leo wana hili kesho wana lile. Kwa ujumla watu hawa huwa hawajipendi na utawajua kwa kauli zao. Siku zote hutamka "heri nife" au "bora damu imwagike" au "piga ua lazima kieleweke" au "ama zao ama zangu"au "sikubali labda niwe maiti" n.k. wote ni ubinafsi na kutoshaurika.
Jamii yetu inahitaji kujiwekea mipango mizuri kimaadili na kitaaluma katika kuhakikisha inajijengea na kujiimarishia uzalendo katika ngazi zote ili vizazi vyetu vipende jamii zao. Jamii zetu zikubali matatizo yaliyopo na ziwe tayari kukabiliana na matatizo hayo. Haitusaidii sana kujuta wala kulaumu. Changamoto kila mahali zipo na zinahitaji kupokelewa na kufanyiwa kazi.
Utamaduni wa mtu leo kukosa hela ya bia anakwenda anapita anakashifu serikali, anamkashifu mungu na kila aliyeko mbele yake si utamaduni wa kutufaa. Hata ukijifanya wewe ni msomali, kama ni mnyaturu utabaki kuwa mnyaturu. Hata ukijipendekeza kwa Obama kama wewe ni wa Kikwete utabaki kuwa wa Kikwete. Sema utakavyosema ukae ukijua kuwa maji ya moto hayachomi nyumba na nanihii ya kuazima haisitiri nanihii.
Hakuna sifa zaidi ya uzalendo. Kujitambua na kujipenda. Jasiri haachi asili. Na ukimsikia mtu anabwata na kujijutia juwa huyo ni maiti anayetembea.

No comments:

Post a Comment