Friday 23 March 2012



AKILI NI NYWELE

Kazi kubwa ya baba na mama ni kuzaa watoto. Wengi wetu tunaisahau kazi hii na kudhani kuwa kazi kubwa ya baba ni kununua gari, kujenga nyumba n.k.
Lazima tukubali kuwa bila ya kuwepo mtoto ubaba na umama unakuwa unatiliwa shaka ama unakuwa haupo kabisa. Mtu atajiita baba kwa ubaba upi ama atajiita mama kwa umama upi; kwa sababu baba au mama anatengenezwa na mtoto.
Kama tunakubaliana kwa hilo, basi na mtoto nae ajue kuwa bila mama na baba yeye asingelikuwepo. Kwa maneno mengine  mtoto anatakiwa awe na staha na heshima kwa wazazi wake. Heshima hii hatakiwi aiuze au abembelezwe kuitoa, huo ni wajibu wake.
Sasa kuna tatizo ambalo sasa hivi linaanza kushamiri la usawa na demokrasia. Kwamba mtoto ameanza kudai haki sawa na mzazi wake na zaidi kutaka awe sawa na wazazi wake. Kwa hilo mtoto anaweza kujaribu, lakini mwisho wa siku atakuta haiwezekani.
Jitihada za watoto kutaka usawa na wazazi wao ndiko ambako kumeanza kuyaporomosha maadili kwa kasi kubwa. Uwazi ambao unafagiliwa sasa hivi unaanza kututumbukia nyongo na kuichefua jamii yetu. Kwa ujumla heshima miongoni mwa wanajamii imeshuka sana.
Tunashuhudia sasa jinsi mjukuu anavyotaka usawa na nyanya yake kwa kutaka kutembea na babu yake, tunashuhudia mtoto wa kiume anavyotaka kumtawala mama yake kama afanyavyo baba yake. Tunashuhudia binti anavyokwenda out na baba yake kama anavyofanya mama yake, na tunashuhudia mwanafunzi anayemkopesha mwalimu wake malaki ya pesa kwa riba. Kesho ni siku ya mtihani, mwalimu huyo anayedaiwa atamlipa nini mwanafunzi wake ?
Watoto wa shule za msingi sasa hivi wana taaluma ya hali ya juu ya mapenzi kushinda hata mama zao na baba zao. Wazazi nao wamekuwa wakipokea amri kutoka kwa watoto wao. Watoto wa sasa wanafanya mambo kwa masharti, bila mzazi kumtimizia atakavyo hilo jambo haliwezekaniki. Jamii yatu imekuwa kama ya kambare, kila mmoja ana sharubu. Mzazi akitaka kutumisha misuri kwa mtoto usikute akaishia jela. Sheria za sasa ni moto wa kuotea mbali.
Hivi katika haki zilizotajwa kwa watoto kutendewa, kumegisiwa wajibu wao kutenda. Tusije tukajikuta tunaingizwa mjini na wanaharakati. Miji mingine ukishaingia, hata kama ni kwa makosa si rahisi ukatoka.

 


 

TATIZO LA KUTOTHUBUTU





Chamwingi Mpondachuma then photo thumbnail



Katika hali inayotia shaka sasa hivi kumekuwa na uzito mkubwa wa watu kutothubutu kutenda japo mambo madogo yaliyo ndani ya uwezo wao. Wengi sasa hivi wamekuwa ni watu wa kulaumu na kusubiri mambo yatendwe na hasa yakosewe ili waweze kuchonga midomo kujitahidi kuonekana kuwa wao hawahusiki. Tabia hii mbali na kutuzidishia umaskini, imekuwa ni kero kiasi  cha hata kuanza kutishia amani.
Tujaribu kujiuliza, hivi tabia hii ingelikuwepo hapo zamani tungeliweza kufikia hatua hii ya dunia kuwa kijiji kimoja ? Kweli kama kila mtu wa enzi hizo angelikuwa na msimamo finyu kama tulivyo wengi kwa sasa maendeleo tunayoyafuja sasa hivi yangelipatikana.
Ni ajabu sasa hivi kuwashuhudia watu kwa makundi wakishinda wanabishana na kulaumu pasi na japo kuchangia chochote na hasa kivitendo katika kuisongesha jamii hii mbele. Imekuwa kama kanuni kila mtu kujitahidi kuhakikisha anavuna lukuki kutoka katika mashamba ambayo hakupanda.
Kwa mwenendo huu ni wazi kuwa hatima ya dunia yetu ipo mashakani na iwe iwavyo atakayepata hasara ni sisi tutakaokutwa na gharika hiyo ya kuteketea ulimwengu ambako kutasababishwa na uzembe wetu wa kutothubutu lakini kuwa watakaji wakubwa wa dezo.



No comments:

Post a Comment