Tuesday 27 March 2012


KUSEMA UZUSHI MBELE YA HADHARA



Duniani kuna watu wa ajabu sana. Wapo watu ambao nyuso zao hazikuumbwa na haya na wala hawana woga. Wao kila wapitako hudhani wanakutana na watoto wadogo ama kudhani wanaongea na mataahira.


Utamkuta mtu ndani ya basi anaanza kwa kusema kuwa serikali yetu imefilisika mpaka imefikia mahali pa kuanza kuuza ardhi kwa majirani. Ataendelea kwa kusema kuwa serikali imeamua kuuuza wilaya za Kasulu na Kibondo kwa nchi ya Burundi na imefanya hivyo ili ipate fedha za kuwalipa madaktari waliogoma. Na kuendelea kueleza kuwa baada ya fedha kupatikana imewalipa madaktari madai yao yote na ndiyo maana wameamua kurejea kamazini.

Anaweza kupita eneo akiwa ndani ya gari na kuona magari yamegongana. Anakokwenda ataanza hadithi kuwa leo amekuta ajali mbaya sana ya gari na maiti za watu karibia kumi zimezagaa barabarani kumbe kaona vipande vya vioo na matone ya damu tu.
Au utamkuta Bar anatangaza kuwa Marekani imepeleka majeshi yake nchini China kupigana baada ya Obama kuona wachina wamekuja juu kiteknolojia.

Ama utamsikia anaongea feri na washkaji zake kuwa Raisi Bush kesho anakuja nchini kulipa pesa za kuinunua Kigamboni yote na wakazi wa Kigamboni inasemekana wametengewa eneo sehemu moja inayoitwa Texas huko Marekani ambapo tayari wamejengewa nyumba na kupatiwa sehemu za kulima.

Mwingine utamkuta anatangaza kuwa CAF imeamua mechi kati ya Yanga na Zamareck itachezwa mjini  Nairobi na baadae Lusaka kutokana na hali ya usalama ya Misri na matatizo ya migomo ya madaktari ya Tanzania.

Watu wa aina hii wanapotokea kuwakuta watu mbumbumbu hufanikiwa kuupotosha umma na kuuafanya uvumi waliousema kusambaa; kumbe ni uzushi na uongo mtupu.

No comments:

Post a Comment