Wednesday 21 March 2012


STAREHE YAKO ISIWE KERO KWA WENGINE


naked drunk woman


Kama tujuavyo, hapa duniani kila mtu ana kitu au jambo analolipenda kulifanya kwa lengo la kuburudisha nafsi yake. Kwanza si vibaya kufanya hivyo.


Tatizo lililopo ni ile starehe ambayo mtu anaitumia kugeuka kuwa kero kwa wengine. Wapo wanaofahamu hilo na wapo wasiofahamu hilo.
Utamkuta mtu ni mpenzi wa mpira wa miguu. Kutokana na mapenzi yake hayo anajikuta kila apitapo na kila amkutaye yeye hana maongezi mengine zaidi ya mambo ya mpira. Na anapokuwa akiongea huwa hana simile wala kituo. Mwanzoni watu humvumilia, lakini baada ya muda anaowasimulia huchoshwa na maongezi yake. Ataaanza na mechi ya Simba na Azam, atakuja usajili wa dirisha dogo ligi ya Uingereza, atahamia kombe la CAN, ataendelea na uchaguzi wa DRFA, ataendelea na kuendelea mpaka watu wamsambae.
Wengine ni wavuta sigara. Utamkuta mtu kazingukwa na kundi la watu ananunua gazeti na kuanza kulisoma. Mara anawasha sigara na kuiacha ikiungua bila kuivuta, ikiisha anawasha nyingine inaendelea kusambaza moshi wakati yeye anasoma gazeti. Hafikirii kuwa ule moshi unawakera wengine. Na sijui ni kwa nini asivute kwanza kisha aendelee na kusoma gazeti. Ama asiende kando kuvuta Hata watu wanapotokea kukohoa kwa ajili ya huo moshi hastuki wala hajali. Na ole wako ujaribu kumweleza kuwa unakerwa na sigara yake; utajuta kuzaliwa.
Wengine ni watu wa mitungi. Atakwenda baa na heshima yake. Atakunywa kupita kiasi hadi kushindwa kuamka katika kiti. Matokeo anajisaidia hapo hapo na kudondosha meza na viti, atavunja glasi na chupa za watu.  Wakati mwingine hulazimika kubebwa kupelekwa kwao. Na akifika kwao ni matusi mtaa mzima. Anapanda kitandani na viatu, anatapikia watoto na mambo chungu nzima ya kuudhi.
Wapo na ndugu zangu wa uswazi. Siku kwake ama kwa jirani kuna ngoma inakuwa hatari kubwa. Mama mzima atayakata mauno utadhani hana akili nzuri. Wengine hujimwaga kwa kupunguza nguo moja hadi nyingine mpaka kubaki karibu na kama alivyozaliwa. Waalikwa hubaki vinywa wazi wasijue waondoke kwenye sherehe ama wabaki maana wamekuja na watoto wao ama dada na kaka zao. Asipotokea mtu wa kuingilia kati vioja hivyo huendelea na kuendelea isivyo kifani.
Hiyo ni mifano michache sana ya baadhi ya watu kujisahau na kustarehe kupita kiasi bila ya kujali maslahi ya wenzao.
Tabia kama hizi kwa hakika hazifai. Kama kwako wewe ni halali, huwezi jua pengine kwa wenzako ni haramu. Tujirekebishe.

SIRI YA SALAMU






Watu wengi hawajui siri ya salamu; na laiti wangewliijua wengi wasingelikuwa kama walivyo.

Siri kubwa ya salamu ni kuwa kipimo tosha cha utu na ustaarabu wa mtu. Ukitaka kumjua mtu aliye mbele yako kuwa ni mwungwana ama mstaarabu basi mpime kwa salamu. Kipimo hiki ni cha uhakika na cha kuaminika sana.
Mtu yeyote ambaye ni mstaarabu hana mizengwe katika salamu. Ni mwepesi wa kusalimia na mchangamfu wa kupokea salamu aliyopewa. Kamwe hawezi kumpita, au kumkuta mtu na akaridhika kuwa karibu naye bila kwanza kumsalimia. Mwungwana hamung'unyi maneno pindi anapokuwa anapokea salamu ama anaposalimia. Salamu yake utaisikia neno kwa neno.
Mstaarabu siku zote hufuata kanuni za salamu.
Kwa kawaida mtu husalimia pale anapomkuta mwenziwe. Husalimia anapowakuta wakubwa hata wadogo kwa salamu zinazowahusu. Husalimia anapokuwa katika chombo cha usafiri kwa mtu aendaye kwa miguu. Husalimia walio ndani wakati yeye yuko nje. Husalimia wa juu wakati yeye yuko chini. Vivyo hivyo hupokea salamu za maskini wakati yeye ni tajiri. Hupokea salamu za wadogo wakati yeye ni mkubwa. hupokea salamu za wa nje wakat yeye yuko ndani. Hupokea salamu waliomkuta.
Ipo mijitu muzito kupokea salamu na aidha huwa haipokei kabisa. Ipo mijitu haitoi salamu mpaka ikumbushwe kila wakati. Ipo mijitu kila siku inapenda ianze kusalimiwa yenyewe tu lakini katu haianzi kusalimia. Naiita mijitu kwa sababu imepungukiwa utu.
Salamu haina duka, haimtoi mtu damu wala haimnyang'anyi mtu cheo wala kumpunguzia mtu utajiri wake. Iweje salamu ikawa nzito kama mzigo.
Ukiona kuna tatizo la salamu kwa mtu ujuege huyo mtu ana walakini. Hiyo ndiyo siri ya salamu.

1 month ago

No comments:

Post a Comment