Friday 13 April 2012


USIRI WA FREEMASON NA MASHAKA YA JAMII


 Kwa kupindi kirefu wengi wetu tumekuwa tukisikia hadithi za kusisimua za Free Mason. Nasema za kusisimua kwa sababu zinasimulia mambo ya kutisha na ya ajabu ambayo yanaogopesha.

Binafsi sijampata mtu wa uhakika wa kunieleza vilivyo kuhusu kitu hiki Free Masom. Kiasi nashindwa kujua kama kundi hili ni la kidini, kichawi, kifisadi ama vipi. Nasema kundi hili linachanganya watu kwa sababu linasemekama lina mchanganyiko wa dini zote, makabila yote, jinsia zote isipokuwa kiuchumi, linachagua wenye mafanikio.

Kama kweli kundi hili si hatari kwa jamii, na kama kweli mambo yake ni mema ni kwanini halijiweki wazi. Usiri wa kundi hili unadhihirisha pengine kuna mambo ya aibu ambayo wanachama wake wanaogopa kama watajulikana  katika jamii itawaharibia  na kuwafanya wakimbiwe ama kuepukwa. Sijapata kumwona mtu hapa kwetu akijinadi kuwa yeye ni mwanachama hai wa kundi hilo. Kuna ubaya gani wa kujulikana kuwa mhusika. Mbona  wenye ukimwi wamejitokeza hadharani. Mbona walokole wanajinadi kila siku.  Kama hawaui, hawamwibii mtu na ni kundi la kusaidiana; wanapojifichaficha hawa wenzetu wanaogopa nini ? 

Hapo kipindi cha nyuma kidogo kulikuwa na afadhari; lakini sasa hivi  kumekuwa kila uchao kukitolewa orodha ya wanachama wa Free Mason wa kitanzania. Kwa jinsi orodha hiyo inavyopanuka kwa kasi nina hofu iko siku hata mimi mwenyewe nitasutwa na Ufree Mason. Sasa hivi kila mwenye mafanikio kifedha na madaraka anatajwa kuwa ni mwanachama wa Free Mason.

Nilidhani kwa nia njema wenzetu wa Free Mason wangelituweka sawa na kututoa wasiwasi kwa kutueleza bayana na waziwazi juu ya shughuli zao na majukumu yao au malengo yao ili kama kikundi kina neema basi wenye kuhitaji waingie. Haifurahishi kukaa kimya bila kusema chochote wakati jamii inawatuhumu kwa kila tukio baya hasa yahusuyo umwagaji damu. Sasa hivi basi likipata ajali na kuua watu kadhaa unaambiwa hiyo kazi ya Free Mason. Meli ikizama usemi ni uleule. Kifo cha kutatanisha cha mtu maarufu, madai hi hayohayo. Kwa hiyo jamii ielewe kuwa tuhuma hizo ni kweli ?

Thursday 12 April 2012




KIFO CHA KANUMBA

KULIA TU HAITOSHI BALI TUJIFUNZE KITU





 Tukumbuke daima kila limpatalo binadamu ni fundisho; fundisho kwake kama yu hai ama fundisho kwa waliobaki hai. Watu kumjadili marehemu Kanumba ama Lulu si kosa, ili mradi iwe ni kwa lengo la kujifunza. Wanapaswa waliobaki au tuliobaki tujue nini cha kupunguza ama nini cha kuongeza katika maisha yetu ili tupate ama yasitukute ya Lulu na Kanumba. Watu huhoji palipo na tukio lisilo la
kawaida na hukaa kimya pale penye tukio lililo la kawaida. Mijadala mingi imeshamiri kutokana na tukio zima la kifo cha Kanumba. Kifo cha Kanumba ni cha aina yake. Mahakama na ifanye kazi yake kwa uwezo wake, lakini na sisi tusizibane midomo katika kulitafakari tukio hili. Ebu fikiria, Lulu binti mdogo wa miaka 19 ak.a. 17 amekwenda kwa mpenzi wake a.k.a. mchumba wake a.k.a. msanii mwenzake. Huko nyumbani kumetokea majibizano a.k.a. ugomvi a.k.a msukumano. Lulu kuona Mpenzi a.k.a Mshkaji kadondoka anatoka na kuondoka; anaacha kisanga kwa ndugu yake. Hasubiri kujua hatma ya hali ya majeruhi ambaye ni kipenzi chake  kama ana hitaji msaada wa kukimbizwa hospitali ama huduma ya kwanza. Pengine alikuwa anawahi daladala, tax, ama anafuata gari aliloacha nje aje ambebe ama alikuwa ana kimbia so ama vyovyote vile. Laiti angelitulia na kuangua kilio pale penye tukio na kujutia mbele ya shemeji yake kwa kueleza ilivyokuwa n.k. maswali na udadisi wa akina yakhe usingelikuwa mkubwa. Yawezekana kwa udogo wa umri wake aliona hivyo ndivyo inafaa; lakini Lulu kama alivyokuwa marehemu Kanumba ni maarufu na watu wanamjua kwa kiasi kikubwa; hivyo wana nafasi ya kumweka katika fungu lolote wanaloona linafaa. Sasa wale wanaojifanya hawayaoni yote haya tuwaweke katika kundi gani....la waungwana, wastaarabu ama ndo walewale ? Pole sana Lulu na Mungu ailaze roho ya marehemu Kanumba mahali pema peponi.... Amen. Lakini ni ukweli usiopingika kuwa kifo hiki kimefundisha wengi mambo mengi.

Friday 30 March 2012


KAZI  USIYOITAKA UNAIOMBA YA NINI ?




Kutokana na hali ilivyokithiri imebidi niongelee hili pia kwani kwa hakika wengi wetu linatukera.

Jambo hili ni tabia ya baadhi ya watu ambao wamezagaa katika huduma mbalimbali lakini wana tabia chafu ambazo haziendani na  maadili ya huduma wanazozitoa.







Utamkuta mtu mwanamama au hata baba yuko hoteli kazi yake ni kuhudumia watu kuwasikiliza  waagizacho na kuwaletea wakitakacho lakini yeye daima ni kufanya ndivyo sivyo. Utamkuta sijui ni kwa sababu gani, lakini huwa hasikilizi maagizo hadi mwisho. Mtu ataagiza aletewe wali kwa nyama ya kuku, lakini yeye kama zuzu anamletea ugali kwa samaki. Anapolalamikiwa kuwa hivyo havikuagizwa, bila ya hata aibu huanza mabishano kwamba yeye ni mzoefu wa kazi yake na hawezi kukosea na maneno mengi ya kashfa kwa mteja.










Ama utamkuta dada yuko baa kazi yake kuuza bia. Mteja atafika kwenye baa hiyo, yeye hajali amezama anasoma gazeti la Ijumaa hujku akicheka pekeyake. Mteja akimstua ampe huduma huinuka huku akisonya na kwenda kuleta Kilimanjaro baridi kwa mteja bila ya hata kumuuliza na kumfungulia. Mteja akionyesha kushangaa, mhudumu huyu humbwatukia maneno na kusisitiza kuwa lazima alipie hicho kinywaji.





Ukienda hospitali nako kuna mengine. Watuwanakwenda na mgonjwa mahututi wanahangaika kumshusha kwenye gari, wahudumu na wamekaa wanaongelea kombe la UEFA. Ukiwauliza mbona hawachangamki, wanakujibu kuwa wao hawashughulikii  eneo hilo wasubiriwe wanaohusika. Wenye mgonjwa wakitaka kuchukua machela wambebe mgonjwa wao wanakuja juu na kuwambia hiyo machela ni ya chumba cha maiti wasiiguse. Watu hubaki wameduwaa hawaelewi wafanye nini; maana hawaelekezwi wafa kufahamishwa utaratibu ukoje.

Mambo haya ya huduma mbovu yamezagaa kila kona. Nenda Polisi, nenda mahakamani, nenda sokoni, madukani, mashuleni n.k. Watu wanafanya kazi kama wamelazimishwa. Wanafanya kazi kama wanajitolea kumbe wanalipwa kwa kazi hizo. Sasa jamani ni kwanini watu wanaomba kazi wasizozipenda na wasio na wito nazo ?

Raha Za Baikoko Tanga

Raha Za Baikoko Tanga

Wednesday 28 March 2012





GUBU LINAKERA KUPITILIZA




Katika mambo ambayo binadamu wengi hawawezi kuyavumilia; basi ni gubu.

Mtu mwenye gubu kwa kawaida huwa hana simile, hana subira, hana shukurani, hana huruma, na nadiriki kusema hata dini hana. Mtu mwenye gubu hajui kusamehe, hajui kusahau, hajui kubembeleza; yeye daima ni kulaumu, kulalamika, kusimanga, na kelele kibao. Naweza kusema ni heri ya mkorofi au mpigaji kuliko mwenye gubu.

Mwenye gubu hana dogo, mwenye gubu haridhiki mwenye gubu daima mdomo wake uko wazi unamwaga maneno kama bomba la maji nmachafu.

Mwenye gubu hudhani kuwa yeye ndiye anayejua, yeye ndiye anayeonewa, yeye ndiye mwangalifu; kwa ujumla mwenye gubu ni mbinafsi. Mwenye gubu hamwamini mwingine pamoja na kwamba yeye hujion ndiye anaaminika.

Kama hujawahi kuishi na mwenye gubu huwezi kuyajua haya, lakini kwa wale ambao wamepambana nao wanalijua hili; mwenye gubu ni moto wa kuotea mbali.

Lakini katika wenye gubu, wapo waliozaliwa na gubu hilo na wapo ambao wanatwezwa na mazingira au hali ya maisha kwa wakati ule. Pasmoja na tofauti zao hayuko mwenye nafuu.

Niseme tu kuwa gubu linakondesha haraka kushinda hata njaa.

Tuesday 27 March 2012


 











NYAMA YA KUKU.

1.       Nina swala laniasi, nahitaji msaada,
Limekuwa si rahisi, kwangu imekuwa mada,
Sina hakika nahisi, jibu linanipa shida,
Hasa ni kiungo gani, kitamu nyama ya kuku.

2.       Zinanitoka kamasi, nazidi poteza muda,
Naingiwa wasiwasi, kama nimepanda boda,
Swali limenisha kasi, nimekwama kama uda,
Hasa ni kiungo gani, kitamu nyama ya kuku.

3.       Nilidhani filigisi, amenikanusha dada,
Kasema tamu kiasi, ina harufu ziada,
Shomboye kama girisi, mdomoni inakwida,
Hasa ni kiungo gani, kitamu nyama ya kuku.


4.       Paja nikalinakisi, lapendwa hadi Finida,
Amenipinga Kaisi, amenicheka Sauda,
Eti mimi ndiyo basi, mbumbumbu au labda,
Hasa ni kiungo gani, kitamu nyama ya kuku.

5.       Kuku anao ukwasi, vipande kwake ni ada,
Ukija kwa kinasisi, wa mitandao ya Voda,
Kidari chashika kasi, lakini si kwa Dauda,
Hasa ni kiungo gani kitamu nyama ya kuku.

6.       Kipapatio wadosi, wasema ndio waheda,
Kinaondoa mikosi, wakila na kuburuda,
Lakini kwa makasisi, hakimo kwenye jalada,
Hasa ni kiungo gani, kitamu nyama ya kuku.


7        Amenambia Hamisi, kwa shingo ndio welda,
Akila anajihisi, ameshiba na faida,
Anavua na soksi, na kuimba dadadida,
Hasa ni kiungo gani, kitamu nyama ya kuku.

8.       Makanyagio msosi, wameutaja makada,
Wanywaji kwa magrasi, acha nyinyi wanywa soda,
Kwamba kitu na boksi, kaone kwenye minada,
Hasa ni kiungo gani, kitamu nyama ya kuku.


9        Ndugu zangu wa  Masasi, kabla kuvuka boda,
Ya kichwa wameasisi, wamesifu kina Sada,
Wasema yashinda ngisi, hata uile kwa dida,
Hasa ni kiungo gani, kitamu nyama ya kuku.

10.     Hapa napiga krosi, nisimalize uroda,
Nawaacha waasisi, mnijaze ushuhuda,
Wajue kadamnasi, Kisiju hadi Singida,
Hasa ni kiungo gani , kitamu nyama ya kuku.









VAZI LA TAIFA



Miongoni mwa mambo ambayo ni ya msingi kwa  Taifa letu na wananchi wake ni kuwa na utambulisho ambao utamfanya kila mwananchi wa  nchi hii atakapoonekana basi atambuliwe kuwa ni Mtanzania.

Miongoni mwa mambo hayo ni vazi la Taifa.

Kumekuwa na mawazo mengi juu ya vazi gain linalofaa kuwa vazi la  Taifa. Mimi nami kama Mtanzania sina budi kuchangia juu ya suala hili.

Nimekuwa nikiyaona mavazi mengi yanayopendekezwa kuwa mavazi ya Taifa. Tatizo nililogundua ni kuwa kwa kiasi Fulani tumekuwa nyuma kiubunifu kiasi kwamba mavazi au mitindo mingi inayoonyeshwa au kupendekezwa ni kama tunairudia au kuiiga toka kwa mataifa mengine.
 
Mimi kwa maoni yangu ningelipenda sisi tujikite katika rangi nne kwanza za taifa ambazo ni kijani; kwamba mtu awe huru kushona mtibndo wowote autakao, lakini pindi utakapokuwa umepangilia rangi zetu zote nne za taifa yaani kijani, njano, bluu na nyeusi basi vazi hilo liwe tayari ni la taifa.
 


Pendekezo langu la pili ni kutumia mavazi ya kimasai lakini katika rangi za taifa, basi hilo nalo liwe vazi la Taifa. Nasema hivi si kwamba ninadharau mavazi ya makabila mengine, lakini tutake tusitake, wamasai ndilo kabila pekee ambalo likekuwa na msimamo wa kulinda vazi lao kila waendako na kila waliko bila ya kuyumbishwa na mavazi haya ambayo yamekuwa yakiingia nchini mwetu kila siku. Hivyo Taifa kwa kuwaenzi, ichukue mavazi yao na kuyafanya ni ya Taifa.

 

 

MPENZI SHAIRI

  

Nilikuwa sijasema, siri ya moyoni mwangu,
Ila leo najituma, kutoa ukweli wangu,
Japo moyo waniuma, hiyo si hiari yangu,
Pokea ukweli wangu, Shairi ninakupenda.


KUSEMA UZUSHI MBELE YA HADHARA



Duniani kuna watu wa ajabu sana. Wapo watu ambao nyuso zao hazikuumbwa na haya na wala hawana woga. Wao kila wapitako hudhani wanakutana na watoto wadogo ama kudhani wanaongea na mataahira.


Utamkuta mtu ndani ya basi anaanza kwa kusema kuwa serikali yetu imefilisika mpaka imefikia mahali pa kuanza kuuza ardhi kwa majirani. Ataendelea kwa kusema kuwa serikali imeamua kuuuza wilaya za Kasulu na Kibondo kwa nchi ya Burundi na imefanya hivyo ili ipate fedha za kuwalipa madaktari waliogoma. Na kuendelea kueleza kuwa baada ya fedha kupatikana imewalipa madaktari madai yao yote na ndiyo maana wameamua kurejea kamazini.

Anaweza kupita eneo akiwa ndani ya gari na kuona magari yamegongana. Anakokwenda ataanza hadithi kuwa leo amekuta ajali mbaya sana ya gari na maiti za watu karibia kumi zimezagaa barabarani kumbe kaona vipande vya vioo na matone ya damu tu.
Au utamkuta Bar anatangaza kuwa Marekani imepeleka majeshi yake nchini China kupigana baada ya Obama kuona wachina wamekuja juu kiteknolojia.

Ama utamsikia anaongea feri na washkaji zake kuwa Raisi Bush kesho anakuja nchini kulipa pesa za kuinunua Kigamboni yote na wakazi wa Kigamboni inasemekana wametengewa eneo sehemu moja inayoitwa Texas huko Marekani ambapo tayari wamejengewa nyumba na kupatiwa sehemu za kulima.

Mwingine utamkuta anatangaza kuwa CAF imeamua mechi kati ya Yanga na Zamareck itachezwa mjini  Nairobi na baadae Lusaka kutokana na hali ya usalama ya Misri na matatizo ya migomo ya madaktari ya Tanzania.

Watu wa aina hii wanapotokea kuwakuta watu mbumbumbu hufanikiwa kuupotosha umma na kuuafanya uvumi waliousema kusambaa; kumbe ni uzushi na uongo mtupu.



MAPENZI HAYALAZIMISHWI

 

 Kuna suala moja muhimu ambalo kwa hakika huwa linaleta usumbusu mkubwa kwa wanaokutwa nalo. Suala hili huwa ni la kupendwa.


Ukiangalia kwa haraka utaona kuwa kupendwa ni jambo zuri la lenye neema. Lakini hapo hapo kupendwa katika mgawanyiko wake suala hili hugeuka kero kwa kuuteka uhuru wa mtu na kuwa adha.

Kupendwa ninakoongelea mimi ni yale mahusiano ya ndani ya jinsia mbili. Mahusiano haya huwa ni lulu na tunu pale tu ambapo ipo ridhaa ya pande zote mbili, lakini kinyume cha hapo huwa ni utumwa kwa mmoja anayelazimishwa.

Wapo wakorofi ambao huamini kuwa kwa jinsi walivyo wanaweza kupendwa na mtu yeyote wakati wowote. Na pindi wanapokuta hali ni kinyume cha walivyoterajia huanza vita na mapambano ya kutaka kuhakikisha wanapata upendo walioukusudia.
Utamkuta  mwanamke au mwanamume amempenda mtu, bila kutumia njia za kistaarabu kuyauza mapenzi yake kwa ampendae na kuendesha michakato halali ya kuteka moyo wa ampendae hukurupuka na kujihesabu kuwa tayari na yeye anapendwa au atapendwa. Kwa hisia hizo hizo huendesha harakati za mapenzi wakati huyo apendwaye hana habari, hahitaji, hajisikii na wala hana  ndoto zozote za mahusiano hayo.

Matokeo ya harakati hizi huwa ni visa, manung'uniko, shutuma, matusi, ugomvi na wakati mwingine husababisha hata vifo kwa aidha aliyependwa kuuliwa, ama anayependa kujiua ama wote kuuawa.

Ni kweli kuwa kipendacho moyo ndicho dawa, lakini tunatambua kisichopendwa na moyo ni nini ? Basi tukumbuke pia kuwa kisichopendwa na moyo ni sumu. Mtu  kulazimishwa kutumia kitu usichokitaka ni kama kuabndamishwa na mauti na hasa pale unapoona kuwa unalazimishwa kukereka kwa furaha ya mtu mmoja. Kama hiyo ni rahisi na inavumilika kwanini yeye asivumilie akakaa kimya au kutumia pindi anapogundua au kutambua kuwa anayempenda hana mahitaji nae ?

Kila binadamu ana uhuru wa kuwepo duniani na ana utashi binafsi katika moyo wake. Ni vema watu wakajifunza kuiheshimu hali hii na kuheshimu nafsi za wengine. Ile hali ya ubinafsi na kujipendelea bila kujali faraja ya watu wengine ni ukorofi na haufai kabisa katika jamii. Hayuko mtu ambaye anaweza kuvumilia penda kitu asichoridhika nacho.



Monday 26 March 2012


ASTE ASTE DADA ZETU…….HUKO TUENDAKO……!




Kwa kipindi cha hivi karibuni nimekuwa nikifuatilia nyenendo za shangazi zangu, dada zangu, shemeji zangu na wengine wakwe zangu; ninachokiona kwa hakika ninaingiwa na hofu.

Lazima niseme nineingiwa na hofu; na si mimi peke yangu; tupo wengi.

Hofu hii imekuwa ikinipata sana hasa upande wa burudani. Kwa sasa imekuwa kama kawaida na pengine kugeuka jadi kwa akina mama kupandwa na mori, mzuka na namna utakavyoita pale ambapo burudani hufika kilele.

Haikatazwi mtu kufurahi au kupagawa, lakini sasa imekuwa inapitiliza. Sasa hivi hata kwenye sherehe ndogo tu ya kipuuzi mtu unaogopa kwenda kwani unaweza ukapambana na vituko mpaka ukashangaa.

Waswahili wanasema kila kitu na mahali pake. Lakini pamoja na msemo huo, mama zangu wamekuwa hawaangazi macho kwanza kabla ya kuanza shughuli zao za kuserebuka. Hawaangazi macho kuhakikisha kama wale wanaowaheshimu wapo ama hawapo. Vijana wamekuwa hawajali kama hapa pana wazee, na wazee nao wamekuwa hawaangazi kuona kama hapa pana watoto. Imekuwa kama fasheni kwenye ngoma kuingizwa mambo ya chumbani. Kuvua nguo imekuwa si jambo la ajabu. Masmbo ya kushikana, kulaliana, kutomasana…..eh!

Dada zangu wangelijaribu kidogo kutafakari kwamba miili ya kiafrika si kama ya wazungu. Mzungu anaweza kwenda hata uchi; kwa mwafrika inakuwa kama mdoli unapita. Lakini mswahili akionyesha kiungo chochote nyeti japo kwa mbali, madhara yake yanakuwa makubwa sana. Hiyo ni kwa kuvaa  bado viuno havijakatwa !

Sina uhakika na hali ya baadae ya mwenendo huu, ndiyo maana nawaombeni mama zangu mtuhurumie aste aste……ama mnataka tusije kwenye ngoma mnazocheza ?

Friday 23 March 2012



AKILI NI NYWELE

Kazi kubwa ya baba na mama ni kuzaa watoto. Wengi wetu tunaisahau kazi hii na kudhani kuwa kazi kubwa ya baba ni kununua gari, kujenga nyumba n.k.
Lazima tukubali kuwa bila ya kuwepo mtoto ubaba na umama unakuwa unatiliwa shaka ama unakuwa haupo kabisa. Mtu atajiita baba kwa ubaba upi ama atajiita mama kwa umama upi; kwa sababu baba au mama anatengenezwa na mtoto.
Kama tunakubaliana kwa hilo, basi na mtoto nae ajue kuwa bila mama na baba yeye asingelikuwepo. Kwa maneno mengine  mtoto anatakiwa awe na staha na heshima kwa wazazi wake. Heshima hii hatakiwi aiuze au abembelezwe kuitoa, huo ni wajibu wake.
Sasa kuna tatizo ambalo sasa hivi linaanza kushamiri la usawa na demokrasia. Kwamba mtoto ameanza kudai haki sawa na mzazi wake na zaidi kutaka awe sawa na wazazi wake. Kwa hilo mtoto anaweza kujaribu, lakini mwisho wa siku atakuta haiwezekani.
Jitihada za watoto kutaka usawa na wazazi wao ndiko ambako kumeanza kuyaporomosha maadili kwa kasi kubwa. Uwazi ambao unafagiliwa sasa hivi unaanza kututumbukia nyongo na kuichefua jamii yetu. Kwa ujumla heshima miongoni mwa wanajamii imeshuka sana.
Tunashuhudia sasa jinsi mjukuu anavyotaka usawa na nyanya yake kwa kutaka kutembea na babu yake, tunashuhudia mtoto wa kiume anavyotaka kumtawala mama yake kama afanyavyo baba yake. Tunashuhudia binti anavyokwenda out na baba yake kama anavyofanya mama yake, na tunashuhudia mwanafunzi anayemkopesha mwalimu wake malaki ya pesa kwa riba. Kesho ni siku ya mtihani, mwalimu huyo anayedaiwa atamlipa nini mwanafunzi wake ?
Watoto wa shule za msingi sasa hivi wana taaluma ya hali ya juu ya mapenzi kushinda hata mama zao na baba zao. Wazazi nao wamekuwa wakipokea amri kutoka kwa watoto wao. Watoto wa sasa wanafanya mambo kwa masharti, bila mzazi kumtimizia atakavyo hilo jambo haliwezekaniki. Jamii yatu imekuwa kama ya kambare, kila mmoja ana sharubu. Mzazi akitaka kutumisha misuri kwa mtoto usikute akaishia jela. Sheria za sasa ni moto wa kuotea mbali.
Hivi katika haki zilizotajwa kwa watoto kutendewa, kumegisiwa wajibu wao kutenda. Tusije tukajikuta tunaingizwa mjini na wanaharakati. Miji mingine ukishaingia, hata kama ni kwa makosa si rahisi ukatoka.

 


 

TATIZO LA KUTOTHUBUTU





Chamwingi Mpondachuma then photo thumbnail



Katika hali inayotia shaka sasa hivi kumekuwa na uzito mkubwa wa watu kutothubutu kutenda japo mambo madogo yaliyo ndani ya uwezo wao. Wengi sasa hivi wamekuwa ni watu wa kulaumu na kusubiri mambo yatendwe na hasa yakosewe ili waweze kuchonga midomo kujitahidi kuonekana kuwa wao hawahusiki. Tabia hii mbali na kutuzidishia umaskini, imekuwa ni kero kiasi  cha hata kuanza kutishia amani.
Tujaribu kujiuliza, hivi tabia hii ingelikuwepo hapo zamani tungeliweza kufikia hatua hii ya dunia kuwa kijiji kimoja ? Kweli kama kila mtu wa enzi hizo angelikuwa na msimamo finyu kama tulivyo wengi kwa sasa maendeleo tunayoyafuja sasa hivi yangelipatikana.
Ni ajabu sasa hivi kuwashuhudia watu kwa makundi wakishinda wanabishana na kulaumu pasi na japo kuchangia chochote na hasa kivitendo katika kuisongesha jamii hii mbele. Imekuwa kama kanuni kila mtu kujitahidi kuhakikisha anavuna lukuki kutoka katika mashamba ambayo hakupanda.
Kwa mwenendo huu ni wazi kuwa hatima ya dunia yetu ipo mashakani na iwe iwavyo atakayepata hasara ni sisi tutakaokutwa na gharika hiyo ya kuteketea ulimwengu ambako kutasababishwa na uzembe wetu wa kutothubutu lakini kuwa watakaji wakubwa wa dezo.




UKIHITAJI KUWA MUWAZI







Kuna watu ambao kwa hakika wanashangaza sana. Watu hawa ni watu ambao wana nafsi dhaifu lakini vichwa vigumu. Watu hawa hawana tofauti na maskini jeuri. Aina hii ya watu ni watata na wakati mwingine husababisha matatizo yasiyo ya lazima kwa kugeukia kushoto wakati wanataka kutazama kulia.
Utamkuta mtu katoka kwao hajala na njaa inamuuma. Anakuta kwa jirani au rafiki yake chakula kipi tayari mezani. Anakaribishwa kwa moyo mmoja, lakini yeye ili pengine asionekane mdoezi na ama kwa sababu zake mwenyewe anasema ahsante kwani si muda mrefu ametoka kula; wakati si kweli. Na mungu humheleleza kwa kupiga muayo mkubwa wa njaa unaotoka moshi mbele ya wenyeji wake.


Mvulana atakuwa amempenda msichana. Badala ya kuwa mkweli ataanza na kumsema pembeni kwa maneno ya kejeri na kashfa nyingi wakati rohoni hajiwezi na yu taabani juu ya msichana huyo.
Yapo mambo mengi makubwa na madogo ambayo huwasibu watu katika uhitaji lakini kwa namna ya ajabu watu hao hujikuta wanapingana na nafsi zao.
Sijaelewa bado, kwanini mtu asiseme ukweli wake kuwa anahitaji badala ya kujivunga  kwa kuwa kisebusebu wakati kiroho kikiwa papo.







CHONDE CHONDE  JAMAA ZETU WA MABONDENI…………!








Hali kama hii bado watu wanakaidi kuhama katika mazingila haya. Hivi tatizo ni nini hasa,  ni kutaka kukaa mjini, ama kushi kwa unafuu; kwani pamoja na kuombwa waondoke mabondeni bado wanahisi kama wanaonewa. Sasa siku watakapojikuta wamekufa maji watamlaumu nani ?


Wednesday 21 March 2012



TUMELOGWA KWA FUTIBOLI


Taifa Stars



 Watanzania nadhani tunatakiwa tujiweke sawa kwa ajili ya kazi ya kumtafuta mganga ili atutibu kutokana na ulozi tuliofanyiwa na wazungu na watani zetu wa Afrika ya Magharibi kuwa kusiweze kabisa kucheza futiboli, sisi tuwe ni watu wa mdumange, kiduku, sindimba; labda tukijitahidi sana basi iwe ni raggae ama kwaito.
Lazima tukubali kuwa tumefanywa misukule wa soka kutokana na kuchanganyikiwa kwetu kiasi cha kushindwa tuanze na lipi na lifuatie lipi ili tuweze na sisi kuwa kama wenzetu; japo isiwe kila siku lakini angalau tufike mbali kidogo katika ulimwengu wa kandanda. Yaelekea tumelogwa tuendelee kuwa kichwa cha mwendawazimu daima.
Si siri kuwa tunawajua wakali wa soka wa dunia nzima. Tumeshajua kuwa ili uendelee kisoka unatakiwa ufanye nini. Cha ajabu badala ya kufanya wafanyavyo wenzetu sisi aidha kwa makusudi lakini nadhani ni kwa kulogwa tunafanya kinyume kabisa. Kwetu mpira ni kula na kunywa kwa sana, baada ya kushiba malumbano, matusi, shutuma na mbwembwe.
Nakumbuka siku za nyuma mimi na wenzangu wakeleketwa tulikwenda kwa mganga akatuambia tufanye yafuatayo kama kweli tunataka nchi isinge mbele kimichezo:
1. Tuchague viongozi wapenda soka sio wapenda madaraka kama uncle  kosa ukimchagua anataka abakie hapo milele
2.Tuchague viongozi wanaojua soka sio wanaojua mizengwe
3.Tuchague viongozi wasiokuwa na matumbo(no rushwa and not kwapukwapu)
4.Tuanzishe mashindano ya shule za msingi na sekondari, toka kikata, kiwilaya, kimkoa hadi kitaifa
5.Tuanzishe mashindano ya vyuo, taasisi, wizara n.k. na kwa msisitizo katika majeshi yetu yote hadi zimamoto
6.Tuwe na mashindano ya tarafa, wilaya na mikoa
7.Tuteue shule za michezo kwa kila mkoa na tuwe na vyuo vya michezo japo vitano katika nchi nzima
8.tuwe na chuo kikuu cha michezo tu
9.Tuwe na chuo cha kuzalisha makocha na waamuzi japo kimoja nchini
10.Tuwe na viwanja vya wazi japo viwili kwa miji ya wilaya, vinne kwa miji ya mikoa, na angalau nene kwa miji mikubwa ambako timu mbalimbali zitafanya mazoezi mchana na usiku kutakuwa kukionyeshwa mashindano mbalimbali ya soka duniani bure.
11.TV na redio zetu zirushe matangazo ya mashindano yote ya soka makubwa nchini.
12.Kuwepo na mpango maalum wa kitaifa wa kusambaza vifaa vya michezo mashuleni. Tumwombe Azamu pamoja na kutengeneza juice atengeneze na vifaa vya michezo. Jezi za Azam, mipira ya Azamu na daluga za Azam. Si yeye tu na wenzie akina Azania, Akina Quality Manji na wengineo.
13.Kila mwezi angalau timu mbili za nje zialikwe na TFF kwa ajili ya kuja kuzinoa timu zetu zinazowakilisha nchi. TFF yetu imelala sana tofauti na tunavyotaka iwe.
Baada ya kukamilisha masharti haya tufukie vichwa vya simba, mapembe ya faru na meno ya tembo katika viwanja vyetu vyote ili timu zetu zisifungike pindi zinapocheza nyumbani.
Tukiona mambo bado magumu tukamwome tena ili aangalie wapi tatizo bado lipo.
Lakini toka tutoke kwa mganga huyo tumerudi tumebweteka, kama sio sisi.



STAREHE YAKO ISIWE KERO KWA WENGINE


naked drunk woman


Kama tujuavyo, hapa duniani kila mtu ana kitu au jambo analolipenda kulifanya kwa lengo la kuburudisha nafsi yake. Kwanza si vibaya kufanya hivyo.


Tatizo lililopo ni ile starehe ambayo mtu anaitumia kugeuka kuwa kero kwa wengine. Wapo wanaofahamu hilo na wapo wasiofahamu hilo.
Utamkuta mtu ni mpenzi wa mpira wa miguu. Kutokana na mapenzi yake hayo anajikuta kila apitapo na kila amkutaye yeye hana maongezi mengine zaidi ya mambo ya mpira. Na anapokuwa akiongea huwa hana simile wala kituo. Mwanzoni watu humvumilia, lakini baada ya muda anaowasimulia huchoshwa na maongezi yake. Ataaanza na mechi ya Simba na Azam, atakuja usajili wa dirisha dogo ligi ya Uingereza, atahamia kombe la CAN, ataendelea na uchaguzi wa DRFA, ataendelea na kuendelea mpaka watu wamsambae.
Wengine ni wavuta sigara. Utamkuta mtu kazingukwa na kundi la watu ananunua gazeti na kuanza kulisoma. Mara anawasha sigara na kuiacha ikiungua bila kuivuta, ikiisha anawasha nyingine inaendelea kusambaza moshi wakati yeye anasoma gazeti. Hafikirii kuwa ule moshi unawakera wengine. Na sijui ni kwa nini asivute kwanza kisha aendelee na kusoma gazeti. Ama asiende kando kuvuta Hata watu wanapotokea kukohoa kwa ajili ya huo moshi hastuki wala hajali. Na ole wako ujaribu kumweleza kuwa unakerwa na sigara yake; utajuta kuzaliwa.
Wengine ni watu wa mitungi. Atakwenda baa na heshima yake. Atakunywa kupita kiasi hadi kushindwa kuamka katika kiti. Matokeo anajisaidia hapo hapo na kudondosha meza na viti, atavunja glasi na chupa za watu.  Wakati mwingine hulazimika kubebwa kupelekwa kwao. Na akifika kwao ni matusi mtaa mzima. Anapanda kitandani na viatu, anatapikia watoto na mambo chungu nzima ya kuudhi.
Wapo na ndugu zangu wa uswazi. Siku kwake ama kwa jirani kuna ngoma inakuwa hatari kubwa. Mama mzima atayakata mauno utadhani hana akili nzuri. Wengine hujimwaga kwa kupunguza nguo moja hadi nyingine mpaka kubaki karibu na kama alivyozaliwa. Waalikwa hubaki vinywa wazi wasijue waondoke kwenye sherehe ama wabaki maana wamekuja na watoto wao ama dada na kaka zao. Asipotokea mtu wa kuingilia kati vioja hivyo huendelea na kuendelea isivyo kifani.
Hiyo ni mifano michache sana ya baadhi ya watu kujisahau na kustarehe kupita kiasi bila ya kujali maslahi ya wenzao.
Tabia kama hizi kwa hakika hazifai. Kama kwako wewe ni halali, huwezi jua pengine kwa wenzako ni haramu. Tujirekebishe.

SIRI YA SALAMU






Watu wengi hawajui siri ya salamu; na laiti wangewliijua wengi wasingelikuwa kama walivyo.

Siri kubwa ya salamu ni kuwa kipimo tosha cha utu na ustaarabu wa mtu. Ukitaka kumjua mtu aliye mbele yako kuwa ni mwungwana ama mstaarabu basi mpime kwa salamu. Kipimo hiki ni cha uhakika na cha kuaminika sana.
Mtu yeyote ambaye ni mstaarabu hana mizengwe katika salamu. Ni mwepesi wa kusalimia na mchangamfu wa kupokea salamu aliyopewa. Kamwe hawezi kumpita, au kumkuta mtu na akaridhika kuwa karibu naye bila kwanza kumsalimia. Mwungwana hamung'unyi maneno pindi anapokuwa anapokea salamu ama anaposalimia. Salamu yake utaisikia neno kwa neno.
Mstaarabu siku zote hufuata kanuni za salamu.
Kwa kawaida mtu husalimia pale anapomkuta mwenziwe. Husalimia anapowakuta wakubwa hata wadogo kwa salamu zinazowahusu. Husalimia anapokuwa katika chombo cha usafiri kwa mtu aendaye kwa miguu. Husalimia walio ndani wakati yeye yuko nje. Husalimia wa juu wakati yeye yuko chini. Vivyo hivyo hupokea salamu za maskini wakati yeye ni tajiri. Hupokea salamu za wadogo wakati yeye ni mkubwa. hupokea salamu za wa nje wakat yeye yuko ndani. Hupokea salamu waliomkuta.
Ipo mijitu muzito kupokea salamu na aidha huwa haipokei kabisa. Ipo mijitu haitoi salamu mpaka ikumbushwe kila wakati. Ipo mijitu kila siku inapenda ianze kusalimiwa yenyewe tu lakini katu haianzi kusalimia. Naiita mijitu kwa sababu imepungukiwa utu.
Salamu haina duka, haimtoi mtu damu wala haimnyang'anyi mtu cheo wala kumpunguzia mtu utajiri wake. Iweje salamu ikawa nzito kama mzigo.
Ukiona kuna tatizo la salamu kwa mtu ujuege huyo mtu ana walakini. Hiyo ndiyo siri ya salamu.

1 month ago


UNAPOFIKIA KUJUTIA ASILI YAKO






Kama kuna utumwa na ufukara wa mawazo, basi ni pamoja na panapokuwepo na hisia hii na kufikia kujuta kuwa wa asili fulani.
Hutokea mtu akajuta kimoyomoyo na baadae kujikuta akitamka bayana kuwa anajuta kuwa mwanamume, au anajuta kuwa mhehe, ama anajuta kuwa Mtanzania n.k. Mtu anajikuta anajuta kwa sanabu zake binafsi kiasi cha kuikashfu jamii yake nzima. Mara nyingi hata kile kinachosababisha akajuta huwa kwa ukweli wa mambo hakina msingi. Kujuta wewe kuwa Mtanzania kwa uwingi wake ni kuamini kuwa watanzania wana kasoro.
Unakuta mtu anajuta kuzaliwa mtanzania kwa sababu tu hana kazi au ajira. Anakuwa anawaza kuwa pengine angelizaliwa marekani angelikuwa hana tatizo hilo. Mwingine hujuta kuwa mwanamume kutokana na kuelemewa na majukumu, anawaza kuwa pengine angelizaliwa mwanamke angeliolewa na kuwa tegemezi; lakini hajakaa akafuatilia kuona ni mazito mangapi yanayowakabili wanawake.
Wazo na hisia hizo kidogo zina nafuu lakini inapopindukia na kumkuta mtu anatamka waziwazi tena kwa kujiamini kabisa kuwa ni heri angelizaliwa mbwa uingereza kuliko kuzaliwa mtu Tanzania hapo ndipo kazi inapokuwa kubwa ya ushauri nasaha. Inabidi ufuatilie kwa undani sana ili kujua sababu hasa za mtu huyu kufikia kuona bora awe bobi ugenini kuliko kuwa mwenyeji katika nchi yake.
Waswahili wanasema mtu unapokuwa fukara wa mawazo unakuwa unatisha kushinda hata mwendawazimu. Mwanafunzi wa chuo kuona heri angelizaliwa mbwa Ulaya kutokana na kucheleweshewa mkopo, mwanamume kuona heri angelizaliwa mwanamke kutokana na kushindwa kuihudumia familia yake, mwanamke kuona heri angelizaliwa mwanamume kutokana na kunyanyasika kimapenzi n.k. kukurejesha katika mawazo ya kawaida kunahitajika kazi ya ziada.
Mawazo ya aina hii ni matokeo ya watu kujifungia vioo na kujibinafshia matatizo. Kuona wao ndio wenye matatizo makubwa kushinda watu wote. Kutarajia mazuri tu katika maisha yao. Kujiona wao wako kamili kimawazo na kifikra kiasi cha kutohitaji kujifunza au kupata ushauri kutoka kwa wengine. Daima hatma ya watu hawa kama si kunywa sumu, au kujinyonga huihujumu jamii kwa itikadi zao, vurugu zao, na visasi vyao. Hawa ndio kama wanavyodai wao kuwa ni mbwa wa kizungu ambao wanalazimika kujifanya watu katika jamii yetu. Watu hawa daima huwa hawaishiwi na hoja; huwa leo wana hili kesho wana lile. Kwa ujumla watu hawa huwa hawajipendi na utawajua kwa kauli zao. Siku zote hutamka "heri nife" au "bora damu imwagike" au "piga ua lazima kieleweke" au "ama zao ama zangu"au "sikubali labda niwe maiti" n.k. wote ni ubinafsi na kutoshaurika.
Jamii yetu inahitaji kujiwekea mipango mizuri kimaadili na kitaaluma katika kuhakikisha inajijengea na kujiimarishia uzalendo katika ngazi zote ili vizazi vyetu vipende jamii zao. Jamii zetu zikubali matatizo yaliyopo na ziwe tayari kukabiliana na matatizo hayo. Haitusaidii sana kujuta wala kulaumu. Changamoto kila mahali zipo na zinahitaji kupokelewa na kufanyiwa kazi.
Utamaduni wa mtu leo kukosa hela ya bia anakwenda anapita anakashifu serikali, anamkashifu mungu na kila aliyeko mbele yake si utamaduni wa kutufaa. Hata ukijifanya wewe ni msomali, kama ni mnyaturu utabaki kuwa mnyaturu. Hata ukijipendekeza kwa Obama kama wewe ni wa Kikwete utabaki kuwa wa Kikwete. Sema utakavyosema ukae ukijua kuwa maji ya moto hayachomi nyumba na nanihii ya kuazima haisitiri nanihii.
Hakuna sifa zaidi ya uzalendo. Kujitambua na kujipenda. Jasiri haachi asili. Na ukimsikia mtu anabwata na kujijutia juwa huyo ni maiti anayetembea.

Tuesday 20 March 2012









LENGO LA KUWA UCHI NI NINI ?






 
Japo sikutaka lakini naona upo umuhimu wa kulisema hili. Hili ni lawama ya moja kwa moja kwa baadhi ya mama au dada zetu. Wako huru tunakubali, lakini uhuru wao au uhuru wowote hauna budi kuwa na mipaka.
Katika moja ya matumizi mabaya ya uhuru wa akina mama ni vitendo vya kujirahisi na kupendelea kukaa nusu uchi au wengine uchi kabisa mbele ya kadamnasi kwa kisingizio cha usanii, michezo, huduma, ama ngoma.
Ni mara nyingi sana nimeshuhudia akina dada hawa wakipanda jukwaani kucheza muziki wakiwa wamevaa vitu mfano wa nguo za ndani. Na kwa kuwa pilikapilika za kucheza muziki si ndogo hujikuta kila wakiinua miguu na kujimwaga huku na kule wanabaki wakiwa watupu.  Hufanya hivyo wakati mwingine hata mbele ya watoto mtaani.Wanapokuwa hivyo hudanganywa na mayowe ya watu kuhamanika na kuweweseka, na wao kuamini kabisa kuwa hadhara husika imefurahishwa sana au kupagawa kwa vitendo vyao. Mambo hayo yanapozidi wenye heshima zao kujiondoa mahali pale na kuwaacha wakware waendelee kusuuza nyoyo zao.
Waweza kwenda pia kwenye Hotel ama Bar huko nako kuna vioja vyake. Nadhani watu hawa wanaogopa mkono wa dora vinginevyo wangeliuza vinywaji wakiwa kama walivyozaliwa.
Wapo wengine utawakuta hawapo Bar wala Disko; pengine madukani, kwenye daladala n.k amevaa nguo ambayo haimruhusu kukaa, kuinama, hata kusimama na kushika chuma kwenye basi. Kila anachokifanya anajikuta kawakalia watu uchi. Ninashindwa kuelewa kama watu hawa walipokuwa wakivaa na kutoka nyumbani kwao walikuwa wamekusudia nini; kuwakalia watu uchi, kupendeza, ama kufanya biashara. Yapo maumbile ambayo kwa hakika hayatakiwi kuwa wazi mbele ya kila mtu, lakini wao wanayaanika kama vitunguu sokoni.
Tatizo la macho ni moja, yanapenda kuangalia maasi ama vitu visivyofaa zaidi ya vitu vya kawaida. Sasa ndugu zetu hawa wanapokuwa wamejichanganya katika jamii mara nyingi huwapa wastaarabu wakati mgumu sana kuyadhibiti macho na mawazo yao. Ni kwanini wadada hawa hufanya hivyo. Hivi tusema hawana dini, hawakulelewa vyema ama wakekumbwa na mapepo.
Kama lengo ni biashara kutokana na soko huria ni vema wangeliomba jiji liwatengee sehemu wafanye biashara yao na watulipe kodi. Mbona hatukuti nyanya zinauzwa kanisani, ama nguo zinauzwa hospitali. Lakini wao ukienda sokoni utawakuta. Ukienda kanisani utawakuta. Ukienda sokoni utawakuta. Ukipita barabarani utawakuta; japokuwa  hawajajibandika bei.
Ebu shangazi zangu wapendwa kaeni mtafakari ni wapi hasa tunakopelekana; vinginevyo mtufafanulie mnapokwenda uchi au kukaa uchi lengo hasa huwa ni nini ? Na je endapo mtaacha kutakuwa na madhara gani na kwa nani ?