USIRI WA FREEMASON NA
MASHAKA YA JAMII
Kwa kupindi kirefu wengi wetu tumekuwa
tukisikia hadithi za kusisimua za Free Mason. Nasema za kusisimua kwa sababu
zinasimulia mambo ya kutisha na ya ajabu ambayo yanaogopesha.
Binafsi sijampata mtu wa uhakika wa kunieleza
vilivyo kuhusu kitu hiki Free Masom. Kiasi nashindwa kujua kama kundi hili ni
la kidini, kichawi, kifisadi ama vipi. Nasema kundi hili linachanganya watu kwa
sababu linasemekama lina mchanganyiko wa dini zote, makabila yote, jinsia zote
isipokuwa kiuchumi, linachagua wenye mafanikio.
Kama kweli kundi hili si hatari kwa jamii,
na kama kweli mambo yake ni mema ni kwanini
halijiweki wazi. Usiri wa kundi hili unadhihirisha pengine kuna mambo ya aibu
ambayo wanachama wake wanaogopa kama
watajulikana katika jamii itawaharibia na kuwafanya wakimbiwe ama kuepukwa. Sijapata
kumwona mtu hapa kwetu akijinadi kuwa yeye ni mwanachama hai wa kundi hilo . Kuna ubaya gani wa kujulikana kuwa
mhusika. Mbona wenye ukimwi wamejitokeza
hadharani. Mbona walokole wanajinadi kila siku.
Kama hawaui, hawamwibii mtu na ni kundi la kusaidiana;
wanapojifichaficha hawa wenzetu wanaogopa nini ?
Hapo kipindi cha nyuma kidogo kulikuwa na
afadhari; lakini sasa hivi kumekuwa kila
uchao kukitolewa orodha ya wanachama wa Free Mason wa kitanzania. Kwa jinsi
orodha hiyo inavyopanuka kwa kasi nina hofu iko siku hata mimi mwenyewe
nitasutwa na Ufree Mason. Sasa hivi kila mwenye mafanikio kifedha na madaraka
anatajwa kuwa ni mwanachama wa Free Mason.
Nilidhani kwa nia njema wenzetu wa Free
Mason wangelituweka sawa na kututoa wasiwasi kwa kutueleza bayana na waziwazi
juu ya shughuli zao na majukumu yao au malengo yao ili kama kikundi kina neema
basi wenye kuhitaji waingie. Haifurahishi kukaa kimya bila kusema chochote
wakati jamii inawatuhumu kwa kila tukio baya hasa yahusuyo umwagaji damu. Sasa
hivi basi likipata ajali na kuua watu kadhaa unaambiwa hiyo kazi ya Free Mason.
Meli ikizama usemi ni uleule. Kifo cha kutatanisha cha mtu maarufu, madai hi
hayohayo. Kwa hiyo jamii ielewe kuwa tuhuma hizo ni kweli ?