Friday 13 April 2012


USIRI WA FREEMASON NA MASHAKA YA JAMII


 Kwa kupindi kirefu wengi wetu tumekuwa tukisikia hadithi za kusisimua za Free Mason. Nasema za kusisimua kwa sababu zinasimulia mambo ya kutisha na ya ajabu ambayo yanaogopesha.

Binafsi sijampata mtu wa uhakika wa kunieleza vilivyo kuhusu kitu hiki Free Masom. Kiasi nashindwa kujua kama kundi hili ni la kidini, kichawi, kifisadi ama vipi. Nasema kundi hili linachanganya watu kwa sababu linasemekama lina mchanganyiko wa dini zote, makabila yote, jinsia zote isipokuwa kiuchumi, linachagua wenye mafanikio.

Kama kweli kundi hili si hatari kwa jamii, na kama kweli mambo yake ni mema ni kwanini halijiweki wazi. Usiri wa kundi hili unadhihirisha pengine kuna mambo ya aibu ambayo wanachama wake wanaogopa kama watajulikana  katika jamii itawaharibia  na kuwafanya wakimbiwe ama kuepukwa. Sijapata kumwona mtu hapa kwetu akijinadi kuwa yeye ni mwanachama hai wa kundi hilo. Kuna ubaya gani wa kujulikana kuwa mhusika. Mbona  wenye ukimwi wamejitokeza hadharani. Mbona walokole wanajinadi kila siku.  Kama hawaui, hawamwibii mtu na ni kundi la kusaidiana; wanapojifichaficha hawa wenzetu wanaogopa nini ? 

Hapo kipindi cha nyuma kidogo kulikuwa na afadhari; lakini sasa hivi  kumekuwa kila uchao kukitolewa orodha ya wanachama wa Free Mason wa kitanzania. Kwa jinsi orodha hiyo inavyopanuka kwa kasi nina hofu iko siku hata mimi mwenyewe nitasutwa na Ufree Mason. Sasa hivi kila mwenye mafanikio kifedha na madaraka anatajwa kuwa ni mwanachama wa Free Mason.

Nilidhani kwa nia njema wenzetu wa Free Mason wangelituweka sawa na kututoa wasiwasi kwa kutueleza bayana na waziwazi juu ya shughuli zao na majukumu yao au malengo yao ili kama kikundi kina neema basi wenye kuhitaji waingie. Haifurahishi kukaa kimya bila kusema chochote wakati jamii inawatuhumu kwa kila tukio baya hasa yahusuyo umwagaji damu. Sasa hivi basi likipata ajali na kuua watu kadhaa unaambiwa hiyo kazi ya Free Mason. Meli ikizama usemi ni uleule. Kifo cha kutatanisha cha mtu maarufu, madai hi hayohayo. Kwa hiyo jamii ielewe kuwa tuhuma hizo ni kweli ?

No comments:

Post a Comment