Tunaruhusu watu wachungulie dirishani na kueleza walichokiona. Tunashauri wasiingie ndani kuhofia yatakayowakuta. Tunawaomba waseme ya muhimu kwa jamii na yasiyo muhimu iwe siri yao.
Saturday 31 March 2012
Friday 30 March 2012
KAZI USIYOITAKA UNAIOMBA YA NINI ?
Kutokana na hali ilivyokithiri imebidi
niongelee hili pia kwani kwa hakika wengi wetu linatukera.
Jambo hili ni tabia ya baadhi ya watu ambao
wamezagaa katika huduma mbalimbali lakini wana tabia chafu ambazo haziendani
na maadili ya huduma wanazozitoa.
Utamkuta mtu mwanamama au hata baba yuko
hoteli kazi yake ni kuhudumia watu kuwasikiliza
waagizacho na kuwaletea wakitakacho lakini yeye daima ni kufanya ndivyo
sivyo. Utamkuta sijui ni kwa sababu gani, lakini huwa hasikilizi maagizo hadi
mwisho. Mtu ataagiza aletewe wali kwa nyama ya kuku, lakini yeye kama zuzu anamletea ugali kwa samaki. Anapolalamikiwa
kuwa hivyo havikuagizwa, bila ya hata aibu huanza mabishano kwamba yeye ni
mzoefu wa kazi yake na hawezi kukosea na maneno mengi ya kashfa kwa mteja.
Ama utamkuta dada yuko baa kazi yake kuuza
bia. Mteja atafika kwenye baa hiyo, yeye hajali amezama anasoma gazeti la
Ijumaa hujku akicheka pekeyake. Mteja akimstua ampe huduma huinuka huku
akisonya na kwenda kuleta Kilimanjaro baridi kwa mteja bila ya hata kumuuliza
na kumfungulia. Mteja akionyesha kushangaa, mhudumu huyu humbwatukia maneno na
kusisitiza kuwa lazima alipie hicho kinywaji.
Ukienda hospitali nako kuna mengine.
Watuwanakwenda na mgonjwa mahututi wanahangaika kumshusha kwenye gari, wahudumu
na wamekaa wanaongelea kombe la UEFA. Ukiwauliza mbona hawachangamki,
wanakujibu kuwa wao hawashughulikii eneo
hilo wasubiriwe
wanaohusika. Wenye mgonjwa wakitaka kuchukua machela wambebe mgonjwa wao
wanakuja juu na kuwambia hiyo machela ni ya chumba cha maiti wasiiguse. Watu
hubaki wameduwaa hawaelewi wafanye nini; maana hawaelekezwi wafa kufahamishwa
utaratibu ukoje.
Mambo haya ya huduma mbovu yamezagaa kila
kona. Nenda Polisi, nenda mahakamani, nenda sokoni, madukani, mashuleni n.k.
Watu wanafanya kazi kama wamelazimishwa.
Wanafanya kazi kama wanajitolea kumbe
wanalipwa kwa kazi hizo. Sasa jamani ni kwanini watu wanaomba kazi
wasizozipenda na wasio na wito nazo ?
Wednesday 28 March 2012
GUBU LINAKERA KUPITILIZA
Katika mambo ambayo binadamu wengi hawawezi kuyavumilia; basi ni
gubu.
Mtu mwenye gubu kwa kawaida huwa hana simile, hana subira, hana
shukurani, hana huruma, na nadiriki kusema hata dini hana. Mtu mwenye gubu
hajui kusamehe, hajui kusahau, hajui kubembeleza; yeye daima ni kulaumu,
kulalamika, kusimanga, na kelele kibao. Naweza kusema ni heri ya mkorofi au
mpigaji kuliko mwenye gubu.
Mwenye gubu hana dogo, mwenye gubu haridhiki mwenye gubu daima
mdomo wake uko wazi unamwaga maneno kama bomba
la maji nmachafu.
Mwenye gubu hudhani kuwa yeye ndiye anayejua, yeye ndiye
anayeonewa, yeye ndiye mwangalifu; kwa ujumla mwenye gubu ni mbinafsi. Mwenye
gubu hamwamini mwingine pamoja na kwamba yeye hujion ndiye anaaminika.
Kama hujawahi kuishi na mwenye gubu huwezi kuyajua haya, lakini
kwa wale ambao wamepambana nao wanalijua hili; mwenye gubu ni moto wa kuotea
mbali.
Lakini katika wenye gubu, wapo waliozaliwa na gubu hilo na wapo ambao wanatwezwa na mazingira
au hali ya maisha kwa wakati ule. Pasmoja na tofauti zao hayuko mwenye nafuu.
Niseme tu kuwa gubu linakondesha haraka kushinda hata njaa.
Tuesday 27 March 2012
NYAMA YA KUKU.
1. Nina swala laniasi, nahitaji msaada,
Limekuwa si rahisi, kwangu imekuwa mada,
Sina hakika nahisi, jibu linanipa shida,
Hasa ni
kiungo gani, kitamu nyama ya kuku.
2. Zinanitoka kamasi, nazidi poteza muda,
Naingiwa wasiwasi, kama nimepanda
boda,
Swali limenisha kasi, nimekwama kama
uda,
Hasa ni
kiungo gani, kitamu nyama ya kuku.
3. Nilidhani filigisi, amenikanusha dada,
Kasema tamu kiasi, ina harufu ziada,
Shomboye kama girisi, mdomoni inakwida,
Hasa ni
kiungo gani, kitamu nyama ya kuku.
4. Paja nikalinakisi, lapendwa hadi
Finida,
Amenipinga Kaisi, amenicheka Sauda,
Eti mimi ndiyo basi, mbumbumbu au labda,
Hasa ni
kiungo gani, kitamu nyama ya kuku.
5. Kuku anao ukwasi, vipande kwake ni
ada,
Ukija kwa kinasisi, wa mitandao ya Voda,
Kidari chashika kasi, lakini si kwa Dauda,
Hasa ni
kiungo gani kitamu nyama ya kuku.
6. Kipapatio wadosi, wasema ndio waheda,
Kinaondoa mikosi, wakila na kuburuda,
Lakini kwa makasisi, hakimo kwenye jalada,
Hasa ni
kiungo gani, kitamu nyama ya kuku.
7 Amenambia Hamisi, kwa shingo ndio
welda,
Akila anajihisi, ameshiba na faida,
Anavua na soksi, na kuimba dadadida,
Hasa ni
kiungo gani, kitamu nyama ya kuku.
8. Makanyagio msosi, wameutaja makada,
Wanywaji kwa magrasi, acha nyinyi wanywa soda,
Kwamba kitu na boksi, kaone kwenye minada,
Hasa ni
kiungo gani, kitamu nyama ya kuku.
9 Ndugu zangu wa Masasi, kabla kuvuka boda,
Ya kichwa wameasisi, wamesifu kina Sada,
Wasema yashinda ngisi, hata uile kwa dida,
Hasa ni
kiungo gani, kitamu nyama ya kuku.
10. Hapa napiga krosi, nisimalize uroda,
Nawaacha waasisi, mnijaze ushuhuda,
Wajue kadamnasi, Kisiju hadi Singida,
Hasa ni
kiungo gani , kitamu nyama ya kuku.
VAZI LA TAIFA
Miongoni
mwa mambo ambayo ni ya msingi kwa Taifa
letu na wananchi wake ni kuwa na utambulisho ambao utamfanya kila mwananchi
wa nchi hii atakapoonekana basi
atambuliwe kuwa ni Mtanzania.
Miongoni
mwa mambo hayo ni vazi la Taifa.
Kumekuwa na
mawazo mengi juu ya vazi gain linalofaa kuwa vazi la Taifa. Mimi nami kama
Mtanzania sina budi kuchangia juu ya suala hili.
Nimekuwa nikiyaona mavazi mengi yanayopendekezwa kuwa
mavazi ya Taifa. Tatizo nililogundua ni kuwa kwa kiasi Fulani tumekuwa nyuma
kiubunifu kiasi kwamba mavazi au mitindo mingi inayoonyeshwa au kupendekezwa ni
kama tunairudia au kuiiga toka kwa mataifa
mengine.
Mimi kwa maoni yangu ningelipenda sisi tujikite katika
rangi nne kwanza za taifa ambazo ni kijani; kwamba mtu awe huru kushona mtibndo
wowote autakao, lakini pindi utakapokuwa umepangilia rangi zetu zote nne za
taifa yaani kijani, njano, bluu na nyeusi basi vazi hilo liwe tayari ni la taifa.
Pendekezo
langu la pili ni kutumia mavazi ya kimasai lakini katika rangi za taifa, basi hilo nalo liwe vazi la
Taifa. Nasema hivi si kwamba ninadharau mavazi ya makabila mengine, lakini
tutake tusitake, wamasai ndilo kabila pekee ambalo likekuwa na msimamo wa
kulinda vazi lao kila waendako na kila waliko bila ya kuyumbishwa na mavazi
haya ambayo yamekuwa yakiingia nchini mwetu kila siku. Hivyo Taifa kwa
kuwaenzi, ichukue mavazi yao na kuyafanya ni ya Taifa.
MPENZI SHAIRI
Nilikuwa sijasema, siri ya moyoni
mwangu,
Ila leo najituma, kutoa ukweli wangu,
Japo moyo waniuma, hiyo si hiari yangu,
Pokea ukweli wangu, Shairi ninakupenda.
KUSEMA UZUSHI MBELE YA HADHARA
Duniani kuna watu wa ajabu sana . Wapo watu ambao nyuso zao hazikuumbwa na haya na wala hawana woga. Wao kila wapitako hudhani wanakutana na watoto wadogo ama kudhani wanaongea na mataahira.
Utamkuta mtu ndani ya basi anaanza kwa kusema kuwa serikali yetu imefilisika mpaka imefikia mahali pa kuanza kuuza ardhi kwa majirani. Ataendelea kwa kusema kuwa serikali imeamua kuuuza wilaya za Kasulu na Kibondo kwa nchi ya Burundi na imefanya hivyo ili ipate fedha za kuwalipa madaktari waliogoma. Na kuendelea kueleza kuwa baada ya fedha kupatikana imewalipa madaktari madai yao yote na ndiyo maana wameamua kurejea kamazini.
Anaweza kupita eneo akiwa ndani ya gari na kuona magari yamegongana. Anakokwenda ataanza hadithi kuwa leo amekuta ajali mbaya sana ya gari na maiti za watu karibia kumi zimezagaa barabarani kumbe kaona vipande vya vioo na matone ya damu tu.
Au utamkuta Bar anatangaza kuwa Marekani imepeleka majeshi yake nchini China kupigana baada ya Obama kuona wachina wamekuja juu kiteknolojia.
Ama utamsikia anaongea feri na washkaji zake kuwa Raisi Bush kesho anakuja nchini kulipa pesa za kuinunua Kigamboni yote na wakazi wa Kigamboni inasemekana wametengewa eneo sehemu moja inayoitwa Texas huko Marekani ambapo tayari wamejengewa nyumba na kupatiwa sehemu za kulima.
Mwingine utamkuta anatangaza kuwa CAF imeamua mechi kati ya Yanga na Zamareck itachezwa mjini Nairobi na baadae Lusaka kutokana na hali ya usalama ya Misri na matatizo ya migomo ya madaktari ya Tanzania .
Watu wa aina hii wanapotokea kuwakuta watu mbumbumbu hufanikiwa kuupotosha umma na kuuafanya uvumi waliousema kusambaa; kumbe ni uzushi na uongo mtupu.
MAPENZI HAYALAZIMISHWI
Kuna suala moja muhimu ambalo kwa hakika huwa linaleta usumbusu
mkubwa kwa wanaokutwa nalo. Suala hili huwa ni la kupendwa.
Ukiangalia kwa haraka utaona kuwa kupendwa ni jambo zuri la lenye
neema. Lakini hapo hapo kupendwa katika mgawanyiko wake suala hili hugeuka
kero kwa kuuteka uhuru wa mtu na kuwa adha.
Kupendwa ninakoongelea mimi ni yale mahusiano ya ndani ya jinsia
mbili. Mahusiano haya huwa ni lulu na tunu pale tu ambapo ipo ridhaa ya pande
zote mbili, lakini kinyume cha hapo huwa ni utumwa kwa mmoja anayelazimishwa.
Wapo wakorofi ambao huamini kuwa kwa jinsi walivyo wanaweza
kupendwa na mtu yeyote wakati wowote. Na pindi wanapokuta hali ni kinyume cha
walivyoterajia huanza vita na mapambano ya kutaka kuhakikisha wanapata upendo
walioukusudia.
Utamkuta mwanamke au mwanamume amempenda mtu, bila kutumia
njia za kistaarabu kuyauza mapenzi yake kwa ampendae na kuendesha michakato halali
ya kuteka moyo wa ampendae hukurupuka na kujihesabu kuwa tayari na yeye
anapendwa au atapendwa. Kwa hisia hizo hizo huendesha harakati za mapenzi
wakati huyo apendwaye hana habari, hahitaji, hajisikii na wala hana ndoto
zozote za mahusiano hayo.
Matokeo ya harakati hizi huwa ni visa, manung'uniko, shutuma,
matusi, ugomvi na wakati mwingine husababisha hata vifo kwa aidha aliyependwa
kuuliwa, ama anayependa kujiua ama wote kuuawa.
Ni kweli kuwa kipendacho moyo ndicho dawa, lakini tunatambua
kisichopendwa na moyo ni nini ? Basi tukumbuke pia kuwa kisichopendwa na moyo
ni sumu. Mtu kulazimishwa kutumia kitu usichokitaka ni kama kuabndamishwa na mauti na hasa
pale unapoona kuwa unalazimishwa kukereka kwa furaha ya mtu mmoja. Kama hiyo ni rahisi na inavumilika kwanini
yeye asivumilie akakaa kimya au kutumia pindi anapogundua au kutambua kuwa
anayempenda hana mahitaji nae ?
Kila binadamu ana uhuru wa kuwepo duniani na ana utashi binafsi
katika moyo wake. Ni vema watu wakajifunza kuiheshimu hali hii na kuheshimu
nafsi za wengine. Ile hali ya ubinafsi na kujipendelea bila kujali faraja ya
watu wengine ni ukorofi na haufai kabisa katika jamii. Hayuko mtu ambaye
anaweza kuvumilia penda kitu asichoridhika nacho.
Monday 26 March 2012
ASTE ASTE DADA ZETU…….HUKO
TUENDAKO……!
Kwa kipindi cha hivi karibuni
nimekuwa nikifuatilia nyenendo za shangazi zangu, dada zangu, shemeji zangu na
wengine wakwe zangu; ninachokiona kwa hakika ninaingiwa na hofu.
Lazima niseme nineingiwa na
hofu; na si mimi peke yangu; tupo wengi.
Hofu hii imekuwa ikinipata sana hasa upande wa
burudani. Kwa sasa imekuwa kama kawaida na
pengine kugeuka jadi kwa akina mama kupandwa na mori, mzuka na namna
utakavyoita pale ambapo burudani hufika kilele.
Haikatazwi mtu kufurahi au
kupagawa, lakini sasa imekuwa inapitiliza. Sasa hivi hata kwenye sherehe ndogo
tu ya kipuuzi mtu unaogopa kwenda kwani unaweza ukapambana na vituko mpaka
ukashangaa.
Waswahili wanasema kila kitu
na mahali pake. Lakini pamoja na msemo huo, mama zangu wamekuwa hawaangazi
macho kwanza kabla ya kuanza shughuli zao za kuserebuka. Hawaangazi macho
kuhakikisha kama wale wanaowaheshimu wapo ama
hawapo. Vijana wamekuwa hawajali kama hapa pana wazee, na wazee nao wamekuwa
hawaangazi kuona kama hapa pana watoto.
Imekuwa kama fasheni kwenye ngoma kuingizwa mambo ya chumbani. Kuvua nguo
imekuwa si jambo la ajabu. Masmbo ya kushikana, kulaliana, kutomasana…..eh!
Dada zangu wangelijaribu
kidogo kutafakari kwamba miili ya kiafrika si kama
ya wazungu. Mzungu anaweza kwenda hata uchi; kwa mwafrika inakuwa kama mdoli unapita. Lakini mswahili akionyesha kiungo
chochote nyeti japo kwa mbali, madhara yake yanakuwa makubwa sana . Hiyo ni kwa kuvaa bado viuno havijakatwa !
Sina uhakika na hali ya
baadae ya mwenendo huu, ndiyo maana nawaombeni mama zangu mtuhurumie aste
aste……ama mnataka tusije kwenye ngoma mnazocheza ?
Friday 23 March 2012
AKILI NI NYWELE
Kazi kubwa ya baba na mama ni kuzaa watoto. Wengi wetu tunaisahau
kazi hii na kudhani kuwa kazi kubwa ya baba ni kununua gari, kujenga nyumba
n.k.Lazima tukubali kuwa bila ya kuwepo mtoto ubaba na umama unakuwa unatiliwa shaka ama unakuwa haupo kabisa. Mtu atajiita baba kwa ubaba upi ama atajiita mama kwa umama upi; kwa sababu baba au mama anatengenezwa na mtoto.
Kama tunakubaliana kwa
Sasa kuna tatizo ambalo sasa hivi linaanza kushamiri la usawa na demokrasia. Kwamba mtoto ameanza kudai haki sawa na mzazi wake na zaidi kutaka awe sawa na wazazi wake. Kwa
Jitihada za watoto kutaka usawa na wazazi wao ndiko ambako kumeanza kuyaporomosha maadili kwa kasi kubwa. Uwazi ambao unafagiliwa sasa hivi unaanza kututumbukia nyongo na kuichefua jamii yetu. Kwa ujumla heshima miongoni mwa wanajamii imeshuka
Tunashuhudia sasa jinsi mjukuu anavyotaka usawa na nyanya yake kwa kutaka kutembea na babu yake, tunashuhudia mtoto wa kiume anavyotaka kumtawala mama yake
Watoto wa shule za msingi sasa hivi wana taaluma ya hali ya juu ya mapenzi kushinda hata mama zao na baba zao. Wazazi nao wamekuwa wakipokea amri kutoka kwa watoto wao. Watoto wa sasa wanafanya mambo kwa masharti, bila mzazi kumtimizia atakavyo
Hivi katika haki zilizotajwa kwa watoto kutendewa, kumegisiwa wajibu wao kutenda. Tusije tukajikuta tunaingizwa mjini na wanaharakati. Miji mingine ukishaingia, hata
TATIZO LA KUTOTHUBUTU
Katika hali inayotia shaka sasa hivi kumekuwa na uzito mkubwa wa watu kutothubutu kutenda japo mambo madogo yaliyo ndani ya uwezo wao. Wengi sasa hivi wamekuwa ni watu wa kulaumu na kusubiri mambo yatendwe na hasa yakosewe ili waweze kuchonga midomo kujitahidi kuonekana kuwa wao hawahusiki. Tabia hii mbali na kutuzidishia umaskini, imekuwa ni kero kiasi cha hata kuanza kutishia amani.
Tujaribu kujiuliza, hivi tabia hii ingelikuwepo hapo zamani tungeliweza kufikia hatua hii ya dunia kuwa kijiji kimoja ? Kweli kama kila mtu wa enzi hizo angelikuwa na msimamo finyu
Ni ajabu sasa hivi kuwashuhudia watu kwa makundi wakishinda wanabishana na kulaumu pasi na japo kuchangia chochote na hasa kivitendo katika kuisongesha jamii hii mbele. Imekuwa kama kanuni kila mtu kujitahidi kuhakikisha anavuna lukuki kutoka katika mashamba ambayo hakupanda.
Kwa mwenendo huu ni wazi kuwa hatima ya dunia yetu ipo mashakani na iwe iwavyo atakayepata hasara ni sisi tutakaokutwa na gharika hiyo ya kuteketea ulimwengu ambako kutasababishwa na uzembe wetu wa kutothubutu lakini kuwa watakaji wakubwa wa dezo.
UKIHITAJI KUWA MUWAZI
Kuna watu ambao kwa hakika wanashangaza
Utamkuta mtu katoka kwao hajala na njaa inamuuma. Anakuta kwa jirani au rafiki yake chakula kipi tayari mezani. Anakaribishwa kwa moyo mmoja, lakini yeye ili pengine asionekane mdoezi na ama kwa sababu zake mwenyewe anasema ahsante kwani si muda mrefu ametoka kula; wakati si kweli. Na mungu humheleleza kwa kupiga muayo mkubwa wa njaa unaotoka moshi mbele ya wenyeji wake.
Mvulana atakuwa amempenda msichana. Badala ya kuwa mkweli ataanza na kumsema pembeni kwa maneno ya kejeri na kashfa nyingi wakati rohoni hajiwezi na yu taabani juu ya msichana huyo.
Yapo mambo mengi makubwa na madogo ambayo huwasibu watu katika uhitaji lakini kwa namna ya ajabu watu hao hujikuta wanapingana na nafsi zao.
Sijaelewa bado, kwanini mtu asiseme ukweli wake kuwa anahitaji badala ya kujivunga kwa kuwa kisebusebu wakati kiroho kikiwa papo.
CHONDE CHONDE JAMAA ZETU WA MABONDENI…………!
Hali kama hii bado watu wanakaidi kuhama katika mazingila
haya. Hivi tatizo ni nini hasa, ni kutaka kukaa mjini, ama kushi kwa
unafuu; kwani pamoja na kuombwa waondoke mabondeni bado wanahisi kama wanaonewa. Sasa siku watakapojikuta wamekufa maji
watamlaumu nani ?
Wednesday 21 March 2012
Watanzania nadhani tunatakiwa tujiweke sawa kwa ajili ya kazi ya kumtafuta mganga ili atutibu kutokana na ulozi tuliofanyiwa na wazungu na watani zetu wa Afrika ya Magharibi kuwa kusiweze kabisa kucheza futiboli, sisi tuwe ni watu wa mdumange, kiduku, sindimba; labda tukijitahidi sana basi iwe ni raggae ama kwaito.
Lazima tukubali kuwa tumefanywa misukule wa soka kutokana na kuchanganyikiwa kwetu kiasi cha kushindwa tuanze na lipi na lifuatie lipi ili tuweze na sisi kuwa kama wenzetu; japo isiwe kila siku lakini angalau tufike mbali kidogo katika ulimwengu wa kandanda. Yaelekea tumelogwa tuendelee kuwa kichwa cha mwendawazimu daima.
Si siri kuwa tunawajua wakali wa soka wa dunia nzima. Tumeshajua kuwa ili uendelee kisoka unatakiwa ufanye nini. Cha ajabu badala ya kufanya wafanyavyo wenzetu sisi aidha kwa makusudi lakini nadhani ni kwa kulogwa tunafanya kinyume kabisa. Kwetu mpira ni kula na kunywa kwa sana, baada ya kushiba malumbano, matusi, shutuma na mbwembwe.
Nakumbuka siku za nyuma mimi na wenzangu wakeleketwa tulikwenda kwa mganga akatuambia tufanye yafuatayo kama kweli tunataka nchi isinge mbele kimichezo:
1. Tuchague viongozi wapenda soka sio wapenda madaraka kama uncle kosa ukimchagua anataka abakie hapo milele
2.Tuchague viongozi wanaojua soka sio wanaojua mizengwe
3.Tuchague viongozi wasiokuwa na matumbo(no rushwa and not kwapukwapu)
4.Tuanzishe mashindano ya shule za msingi na sekondari, toka kikata, kiwilaya, kimkoa hadi kitaifa
5.Tuanzishe mashindano ya vyuo, taasisi, wizara n.k. na kwa msisitizo katika majeshi yetu yote hadi zimamoto
6.Tuwe na mashindano ya tarafa, wilaya na mikoa
7.Tuteue shule za michezo kwa kila mkoa na tuwe na vyuo vya michezo japo vitano katika nchi nzima
8.tuwe na chuo kikuu cha michezo tu
9.Tuwe na chuo cha kuzalisha makocha na waamuzi japo kimoja nchini
10.Tuwe na viwanja vya wazi japo viwili kwa miji ya wilaya, vinne kwa miji ya mikoa, na angalau nene kwa miji mikubwa ambako timu mbalimbali zitafanya mazoezi mchana na usiku kutakuwa kukionyeshwa mashindano mbalimbali ya soka duniani bure.
11.TV na redio zetu zirushe matangazo ya mashindano yote ya soka makubwa nchini.
12.Kuwepo na mpango maalum wa kitaifa wa kusambaza vifaa vya michezo mashuleni. Tumwombe Azamu pamoja na kutengeneza juice atengeneze na vifaa vya michezo. Jezi za Azam, mipira ya Azamu na daluga za Azam. Si yeye tu na wenzie akina Azania, Akina Quality Manji na wengineo.
13.Kila mwezi angalau timu mbili za nje zialikwe na TFF kwa ajili ya kuja kuzinoa timu zetu zinazowakilisha nchi. TFF yetu imelala sana tofauti na tunavyotaka iwe.
Baada ya kukamilisha masharti haya tufukie vichwa vya simba, mapembe ya faru na meno ya tembo katika viwanja vyetu vyote ili timu zetu zisifungike pindi zinapocheza nyumbani.
Tukiona mambo bado magumu tukamwome tena ili aangalie wapi tatizo bado lipo.
Lakini toka tutoke kwa mganga huyo tumerudi tumebweteka, kama sio sisi.
STAREHE YAKO ISIWE KERO KWA WENGINE
Kama tujuavyo, hapa duniani kila mtu ana
kitu au jambo analolipenda kulifanya kwa lengo la kuburudisha nafsi yake. Kwanza si vibaya kufanya hivyo.
Tatizo lililopo ni ile starehe ambayo mtu anaitumia kugeuka kuwa kero kwa wengine. Wapo wanaofahamu
Utamkuta mtu ni mpenzi wa mpira wa miguu. Kutokana na mapenzi yake hayo anajikuta kila apitapo na kila amkutaye yeye hana maongezi mengine zaidi ya mambo ya mpira. Na anapokuwa akiongea huwa hana simile wala kituo. Mwanzoni watu humvumilia, lakini baada ya muda anaowasimulia huchoshwa na maongezi yake. Ataaanza na mechi ya Simba na Azam, atakuja usajili wa dirisha dogo ligi ya Uingereza, atahamia kombe la CAN, ataendelea na uchaguzi wa DRFA, ataendelea na kuendelea mpaka watu wamsambae.
Wengine ni wavuta sigara. Utamkuta mtu kazingukwa na kundi la watu ananunua gazeti na kuanza kulisoma. Mara anawasha sigara na kuiacha ikiungua bila kuivuta, ikiisha anawasha nyingine inaendelea kusambaza moshi wakati yeye anasoma gazeti. Hafikirii kuwa ule moshi unawakera wengine. Na sijui ni kwa nini asivute kwanza kisha aendelee na kusoma gazeti. Ama asiende kando kuvuta Hata watu wanapotokea kukohoa kwa ajili ya huo moshi hastuki wala hajali. Na ole wako ujaribu kumweleza kuwa unakerwa na sigara yake; utajuta kuzaliwa.
Wengine ni watu wa mitungi. Atakwenda baa na heshima yake. Atakunywa kupita kiasi hadi kushindwa kuamka katika kiti. Matokeo anajisaidia hapo hapo na kudondosha meza na viti, atavunja glasi na chupa za watu. Wakati mwingine hulazimika kubebwa kupelekwa kwao. Na akifika kwao ni matusi mtaa mzima. Anapanda kitandani na viatu, anatapikia watoto na mambo chungu nzima ya kuudhi.
Wapo na ndugu zangu wa uswazi. Siku kwake ama kwa jirani kuna ngoma inakuwa hatari kubwa. Mama mzima atayakata mauno utadhani hana akili nzuri. Wengine hujimwaga kwa kupunguza nguo moja hadi nyingine mpaka kubaki karibu na
Hiyo ni mifano michache
Tabia kama hizi kwa hakika hazifai.
SIRI YA SALAMU
Watu wengi hawajui siri ya salamu; na laiti wangewliijua wengi wasingelikuwa
Siri kubwa ya salamu ni kuwa kipimo tosha cha utu na ustaarabu wa mtu. Ukitaka kumjua mtu aliye mbele yako kuwa ni mwungwana ama mstaarabu basi mpime kwa salamu. Kipimo hiki ni cha uhakika na cha kuaminika
Mtu yeyote ambaye ni mstaarabu hana mizengwe katika salamu. Ni mwepesi wa kusalimia na mchangamfu wa kupokea salamu aliyopewa. Kamwe hawezi kumpita, au kumkuta mtu na akaridhika kuwa karibu naye bila kwanza kumsalimia. Mwungwana hamung'unyi maneno pindi anapokuwa anapokea salamu ama anaposalimia. Salamu yake utaisikia neno kwa neno.
Mstaarabu siku zote hufuata kanuni za salamu.
Kwa kawaida mtu husalimia pale anapomkuta mwenziwe. Husalimia anapowakuta wakubwa hata wadogo kwa salamu zinazowahusu. Husalimia anapokuwa katika chombo cha usafiri kwa mtu aendaye kwa miguu. Husalimia walio ndani wakati yeye yuko nje. Husalimia wa juu wakati yeye yuko chini. Vivyo hivyo hupokea salamu za maskini wakati yeye ni tajiri. Hupokea salamu za wadogo wakati yeye ni mkubwa. hupokea salamu za wa nje wakat yeye yuko ndani. Hupokea salamu waliomkuta.
Ipo mijitu muzito kupokea salamu na aidha huwa haipokei kabisa. Ipo mijitu haitoi salamu mpaka ikumbushwe kila wakati. Ipo mijitu kila siku inapenda ianze kusalimiwa yenyewe tu lakini katu haianzi kusalimia. Naiita mijitu kwa sababu imepungukiwa utu.
Salamu haina duka, haimtoi mtu damu wala haimnyang'anyi mtu cheo wala kumpunguzia mtu utajiri wake. Iweje salamu ikawa nzito
Ukiona kuna tatizo la salamu kwa mtu ujuege huyo mtu ana walakini. Hiyo ndiyo siri ya salamu.
1 month ago
UNAPOFIKIA KUJUTIA ASILI YAKO
Hutokea mtu akajuta kimoyomoyo na baadae kujikuta akitamka bayana kuwa anajuta kuwa mwanamume, au anajuta kuwa mhehe, ama anajuta kuwa Mtanzania n.k. Mtu anajikuta anajuta kwa sanabu zake binafsi kiasi cha kuikashfu jamii yake nzima. Mara nyingi hata kile kinachosababisha akajuta huwa kwa ukweli wa mambo hakina msingi. Kujuta wewe kuwa Mtanzania kwa uwingi wake ni kuamini kuwa watanzania wana kasoro.
Unakuta mtu anajuta kuzaliwa mtanzania kwa sababu tu hana kazi au ajira. Anakuwa anawaza kuwa pengine angelizaliwa marekani angelikuwa hana tatizo
Wazo na hisia hizo kidogo zina nafuu lakini inapopindukia na kumkuta mtu anatamka waziwazi tena kwa kujiamini kabisa kuwa ni heri angelizaliwa mbwa uingereza kuliko kuzaliwa mtu
Waswahili wanasema mtu unapokuwa fukara wa mawazo unakuwa unatisha kushinda hata mwendawazimu. Mwanafunzi wa chuo kuona heri angelizaliwa mbwa Ulaya kutokana na kucheleweshewa mkopo, mwanamume kuona heri angelizaliwa mwanamke kutokana na kushindwa kuihudumia familia yake, mwanamke kuona heri angelizaliwa mwanamume kutokana na kunyanyasika kimapenzi n.k. kukurejesha katika mawazo ya kawaida kunahitajika kazi ya ziada.
Mawazo ya aina hii ni matokeo ya watu kujifungia vioo na kujibinafshia matatizo. Kuona wao ndio wenye matatizo makubwa kushinda watu wote. Kutarajia mazuri tu katika maisha
Jamii yetu inahitaji kujiwekea mipango mizuri kimaadili na kitaaluma katika kuhakikisha inajijengea na kujiimarishia uzalendo katika ngazi zote ili vizazi vyetu vipende jamii zao. Jamii zetu zikubali matatizo yaliyopo na ziwe tayari kukabiliana na matatizo hayo. Haitusaidii
Utamaduni wa mtu leo kukosa hela ya bia anakwenda anapita anakashifu serikali, anamkashifu mungu na kila aliyeko mbele yake si utamaduni wa kutufaa. Hata ukijifanya wewe ni msomali,
Hakuna sifa zaidi ya uzalendo. Kujitambua na kujipenda. Jasiri haachi asili. Na ukimsikia mtu anabwata na kujijutia juwa huyo ni maiti anayetembea.
Tuesday 20 March 2012
Japo sikutaka lakini naona upo umuhimu wa kulisema hili. Hili ni lawama ya moja kwa moja kwa baadhi ya mama au dada zetu. Wako huru tunakubali, lakini uhuru wao au uhuru wowote hauna budi kuwa na mipaka.
Katika moja ya matumizi mabaya ya uhuru wa akina mama ni vitendo vya kujirahisi na kupendelea kukaa nusu uchi au wengine uchi kabisa mbele ya kadamnasi kwa kisingizio cha usanii, michezo, huduma, ama ngoma.
Ni mara nyingi
Waweza kwenda pia kwenye Hotel ama Bar huko nako kuna vioja vyake. Nadhani watu hawa wanaogopa mkono wa dora vinginevyo wangeliuza vinywaji wakiwa
Wapo wengine utawakuta hawapo Bar wala Disko; pengine madukani, kwenye daladala n.k amevaa nguo ambayo haimruhusu kukaa, kuinama, hata kusimama na kushika chuma kwenye basi. Kila anachokifanya anajikuta kawakalia watu uchi. Ninashindwa kuelewa
Tatizo la macho ni moja, yanapenda kuangalia maasi ama vitu visivyofaa zaidi ya vitu vya kawaida. Sasa ndugu zetu hawa wanapokuwa wamejichanganya katika jamii mara nyingi huwapa wastaarabu wakati mgumu
Kama lengo ni biashara kutokana na soko huria ni vema wangeliomba jiji liwatengee sehemu wafanye biashara
Ebu shangazi zangu wapendwa kaeni mtafakari ni wapi hasa tunakopelekana; vinginevyo mtufafanulie mnapokwenda uchi au kukaa uchi lengo hasa huwa ni nini ? Na je endapo mtaacha kutakuwa na madhara gani na kwa nani ?
AJALI
HAINA KINGA
Siku
zote watu tunapokuwa wazima huwa tunajisahau sana . Huwa tunadhani wanaostahili kupata
ajali ni wengine na sisi hatumo katika orodha hiyo; na wakati mwingine huwa
tunafikia hata kukufuru kwa kudhani waliopata ajali walijitakiwa wenyewe ama ni
wajinga.
Moja
ya maeneo ambayo wengi wetu tumebweteka ni katika vyombo vya usafiri. Laiti
kama mungu asingeliingilia kati na kuachia kila uzembe unaofanyika katika
vyombo vya usafiri uzae matunda, basi nadhani kufikia leo zaidi ya nusu ya
wakazi wa dunia hii wangelikuwa wametoweka kwa ajali.
Utamkuta
dareva amejaza abiria kwenye gari lake
anakwenda mwendo ambao hata kama
itatokezea hitilafu yoyote japo ndogo aidha barabarani ama katika gari lake basi
hatakuwa na namna yoyote ya kuokoa maisha ya watu aliowabeba.
Sambamba
na madereva, na abiria nao mara nyingi wanachangia kwani ni wepesi wa kuhimiza
dareva aende mwendo kasi ili waweze kuwahi waendako ama wakati mwingine ni
asili ya ushabiki usio na sababu wa kupenda mwendo mkali.
Zamani
tatizo lilikuwa katika magari, lakini sasa hivi kumekuja usafiri wa pikipiki au bodaboda. Vyombo hivi vimekuwa ni
hatarishi kiasi ambacho tunaweza kusema ni janga la Taifa. Jamaa waendeshao
vyombo hivi wamekuwa wakorofi barabarani kiasi kwamba maisha yao
wamekwisha yakabidhi mbinguni na wao wanatembea
wakiwa kama maiti watembeao. Bodaboda
hawajali kama kuna kuanguka ama kugonga,
wanachokijua wao ni kufika haraka iwezekanavyo huko waendako.
Abiria
wa bodaboda nao sijui ni kwa sababu ya ukata ama vipi, hulazimisha kupanda
wengi katika pikipiki moja kana kwamba wako
katika mchezo wa sarakasi. Wengine kama si wanene hupanda watatu na
dareva kuwa wane katika pikipiki moja; wenyewe wanaita mishikaki.
Sasa
kama tunafanya uzembe wa makusudi kwa kisingizio cha kuwa ajali haina kinga
tuendelee mpaka yaje kutukuta na hapo ndipo tutakuja kujua kama
ajali ina kinga au haina.
Subscribe to:
Posts (Atom)