NYAMA YA KUKU.
1. Nina swala laniasi, nahitaji msaada,
Limekuwa si rahisi, kwangu imekuwa mada,
Sina hakika nahisi, jibu linanipa shida,
Hasa ni
kiungo gani, kitamu nyama ya kuku.
2. Zinanitoka kamasi, nazidi poteza muda,
Naingiwa wasiwasi, kama nimepanda
boda,
Swali limenisha kasi, nimekwama kama
uda,
Hasa ni
kiungo gani, kitamu nyama ya kuku.
3. Nilidhani filigisi, amenikanusha dada,
Kasema tamu kiasi, ina harufu ziada,
Shomboye kama girisi, mdomoni inakwida,
Hasa ni
kiungo gani, kitamu nyama ya kuku.
4. Paja nikalinakisi, lapendwa hadi
Finida,
Amenipinga Kaisi, amenicheka Sauda,
Eti mimi ndiyo basi, mbumbumbu au labda,
Hasa ni
kiungo gani, kitamu nyama ya kuku.
5. Kuku anao ukwasi, vipande kwake ni
ada,
Ukija kwa kinasisi, wa mitandao ya Voda,
Kidari chashika kasi, lakini si kwa Dauda,
Hasa ni
kiungo gani kitamu nyama ya kuku.
6. Kipapatio wadosi, wasema ndio waheda,
Kinaondoa mikosi, wakila na kuburuda,
Lakini kwa makasisi, hakimo kwenye jalada,
Hasa ni
kiungo gani, kitamu nyama ya kuku.
7 Amenambia Hamisi, kwa shingo ndio
welda,
Akila anajihisi, ameshiba na faida,
Anavua na soksi, na kuimba dadadida,
Hasa ni
kiungo gani, kitamu nyama ya kuku.
8. Makanyagio msosi, wameutaja makada,
Wanywaji kwa magrasi, acha nyinyi wanywa soda,
Kwamba kitu na boksi, kaone kwenye minada,
Hasa ni
kiungo gani, kitamu nyama ya kuku.
9 Ndugu zangu wa Masasi, kabla kuvuka boda,
Ya kichwa wameasisi, wamesifu kina Sada,
Wasema yashinda ngisi, hata uile kwa dida,
Hasa ni
kiungo gani, kitamu nyama ya kuku.
10. Hapa napiga krosi, nisimalize uroda,
Nawaacha waasisi, mnijaze ushuhuda,
Wajue kadamnasi, Kisiju hadi Singida,
Hasa ni
kiungo gani , kitamu nyama ya kuku.
No comments:
Post a Comment