Tuesday 20 March 2012









LENGO LA KUWA UCHI NI NINI ?






 
Japo sikutaka lakini naona upo umuhimu wa kulisema hili. Hili ni lawama ya moja kwa moja kwa baadhi ya mama au dada zetu. Wako huru tunakubali, lakini uhuru wao au uhuru wowote hauna budi kuwa na mipaka.
Katika moja ya matumizi mabaya ya uhuru wa akina mama ni vitendo vya kujirahisi na kupendelea kukaa nusu uchi au wengine uchi kabisa mbele ya kadamnasi kwa kisingizio cha usanii, michezo, huduma, ama ngoma.
Ni mara nyingi sana nimeshuhudia akina dada hawa wakipanda jukwaani kucheza muziki wakiwa wamevaa vitu mfano wa nguo za ndani. Na kwa kuwa pilikapilika za kucheza muziki si ndogo hujikuta kila wakiinua miguu na kujimwaga huku na kule wanabaki wakiwa watupu.  Hufanya hivyo wakati mwingine hata mbele ya watoto mtaani.Wanapokuwa hivyo hudanganywa na mayowe ya watu kuhamanika na kuweweseka, na wao kuamini kabisa kuwa hadhara husika imefurahishwa sana au kupagawa kwa vitendo vyao. Mambo hayo yanapozidi wenye heshima zao kujiondoa mahali pale na kuwaacha wakware waendelee kusuuza nyoyo zao.
Waweza kwenda pia kwenye Hotel ama Bar huko nako kuna vioja vyake. Nadhani watu hawa wanaogopa mkono wa dora vinginevyo wangeliuza vinywaji wakiwa kama walivyozaliwa.
Wapo wengine utawakuta hawapo Bar wala Disko; pengine madukani, kwenye daladala n.k amevaa nguo ambayo haimruhusu kukaa, kuinama, hata kusimama na kushika chuma kwenye basi. Kila anachokifanya anajikuta kawakalia watu uchi. Ninashindwa kuelewa kama watu hawa walipokuwa wakivaa na kutoka nyumbani kwao walikuwa wamekusudia nini; kuwakalia watu uchi, kupendeza, ama kufanya biashara. Yapo maumbile ambayo kwa hakika hayatakiwi kuwa wazi mbele ya kila mtu, lakini wao wanayaanika kama vitunguu sokoni.
Tatizo la macho ni moja, yanapenda kuangalia maasi ama vitu visivyofaa zaidi ya vitu vya kawaida. Sasa ndugu zetu hawa wanapokuwa wamejichanganya katika jamii mara nyingi huwapa wastaarabu wakati mgumu sana kuyadhibiti macho na mawazo yao. Ni kwanini wadada hawa hufanya hivyo. Hivi tusema hawana dini, hawakulelewa vyema ama wakekumbwa na mapepo.
Kama lengo ni biashara kutokana na soko huria ni vema wangeliomba jiji liwatengee sehemu wafanye biashara yao na watulipe kodi. Mbona hatukuti nyanya zinauzwa kanisani, ama nguo zinauzwa hospitali. Lakini wao ukienda sokoni utawakuta. Ukienda kanisani utawakuta. Ukienda sokoni utawakuta. Ukipita barabarani utawakuta; japokuwa  hawajajibandika bei.
Ebu shangazi zangu wapendwa kaeni mtafakari ni wapi hasa tunakopelekana; vinginevyo mtufafanulie mnapokwenda uchi au kukaa uchi lengo hasa huwa ni nini ? Na je endapo mtaacha kutakuwa na madhara gani na kwa nani ?


No comments:

Post a Comment