Tuesday 27 March 2012



MAPENZI HAYALAZIMISHWI

 

 Kuna suala moja muhimu ambalo kwa hakika huwa linaleta usumbusu mkubwa kwa wanaokutwa nalo. Suala hili huwa ni la kupendwa.


Ukiangalia kwa haraka utaona kuwa kupendwa ni jambo zuri la lenye neema. Lakini hapo hapo kupendwa katika mgawanyiko wake suala hili hugeuka kero kwa kuuteka uhuru wa mtu na kuwa adha.

Kupendwa ninakoongelea mimi ni yale mahusiano ya ndani ya jinsia mbili. Mahusiano haya huwa ni lulu na tunu pale tu ambapo ipo ridhaa ya pande zote mbili, lakini kinyume cha hapo huwa ni utumwa kwa mmoja anayelazimishwa.

Wapo wakorofi ambao huamini kuwa kwa jinsi walivyo wanaweza kupendwa na mtu yeyote wakati wowote. Na pindi wanapokuta hali ni kinyume cha walivyoterajia huanza vita na mapambano ya kutaka kuhakikisha wanapata upendo walioukusudia.
Utamkuta  mwanamke au mwanamume amempenda mtu, bila kutumia njia za kistaarabu kuyauza mapenzi yake kwa ampendae na kuendesha michakato halali ya kuteka moyo wa ampendae hukurupuka na kujihesabu kuwa tayari na yeye anapendwa au atapendwa. Kwa hisia hizo hizo huendesha harakati za mapenzi wakati huyo apendwaye hana habari, hahitaji, hajisikii na wala hana  ndoto zozote za mahusiano hayo.

Matokeo ya harakati hizi huwa ni visa, manung'uniko, shutuma, matusi, ugomvi na wakati mwingine husababisha hata vifo kwa aidha aliyependwa kuuliwa, ama anayependa kujiua ama wote kuuawa.

Ni kweli kuwa kipendacho moyo ndicho dawa, lakini tunatambua kisichopendwa na moyo ni nini ? Basi tukumbuke pia kuwa kisichopendwa na moyo ni sumu. Mtu  kulazimishwa kutumia kitu usichokitaka ni kama kuabndamishwa na mauti na hasa pale unapoona kuwa unalazimishwa kukereka kwa furaha ya mtu mmoja. Kama hiyo ni rahisi na inavumilika kwanini yeye asivumilie akakaa kimya au kutumia pindi anapogundua au kutambua kuwa anayempenda hana mahitaji nae ?

Kila binadamu ana uhuru wa kuwepo duniani na ana utashi binafsi katika moyo wake. Ni vema watu wakajifunza kuiheshimu hali hii na kuheshimu nafsi za wengine. Ile hali ya ubinafsi na kujipendelea bila kujali faraja ya watu wengine ni ukorofi na haufai kabisa katika jamii. Hayuko mtu ambaye anaweza kuvumilia penda kitu asichoridhika nacho.



No comments:

Post a Comment