KAZI USIYOITAKA UNAIOMBA YA NINI ?
Kutokana na hali ilivyokithiri imebidi
niongelee hili pia kwani kwa hakika wengi wetu linatukera.
Jambo hili ni tabia ya baadhi ya watu ambao
wamezagaa katika huduma mbalimbali lakini wana tabia chafu ambazo haziendani
na maadili ya huduma wanazozitoa.
Utamkuta mtu mwanamama au hata baba yuko
hoteli kazi yake ni kuhudumia watu kuwasikiliza
waagizacho na kuwaletea wakitakacho lakini yeye daima ni kufanya ndivyo
sivyo. Utamkuta sijui ni kwa sababu gani, lakini huwa hasikilizi maagizo hadi
mwisho. Mtu ataagiza aletewe wali kwa nyama ya kuku, lakini yeye kama zuzu anamletea ugali kwa samaki. Anapolalamikiwa
kuwa hivyo havikuagizwa, bila ya hata aibu huanza mabishano kwamba yeye ni
mzoefu wa kazi yake na hawezi kukosea na maneno mengi ya kashfa kwa mteja.
Ama utamkuta dada yuko baa kazi yake kuuza
bia. Mteja atafika kwenye baa hiyo, yeye hajali amezama anasoma gazeti la
Ijumaa hujku akicheka pekeyake. Mteja akimstua ampe huduma huinuka huku
akisonya na kwenda kuleta Kilimanjaro baridi kwa mteja bila ya hata kumuuliza
na kumfungulia. Mteja akionyesha kushangaa, mhudumu huyu humbwatukia maneno na
kusisitiza kuwa lazima alipie hicho kinywaji.
Ukienda hospitali nako kuna mengine.
Watuwanakwenda na mgonjwa mahututi wanahangaika kumshusha kwenye gari, wahudumu
na wamekaa wanaongelea kombe la UEFA. Ukiwauliza mbona hawachangamki,
wanakujibu kuwa wao hawashughulikii eneo
hilo wasubiriwe
wanaohusika. Wenye mgonjwa wakitaka kuchukua machela wambebe mgonjwa wao
wanakuja juu na kuwambia hiyo machela ni ya chumba cha maiti wasiiguse. Watu
hubaki wameduwaa hawaelewi wafanye nini; maana hawaelekezwi wafa kufahamishwa
utaratibu ukoje.
Mambo haya ya huduma mbovu yamezagaa kila
kona. Nenda Polisi, nenda mahakamani, nenda sokoni, madukani, mashuleni n.k.
Watu wanafanya kazi kama wamelazimishwa.
Wanafanya kazi kama wanajitolea kumbe
wanalipwa kwa kazi hizo. Sasa jamani ni kwanini watu wanaomba kazi
wasizozipenda na wasio na wito nazo ?
No comments:
Post a Comment