Tuesday 20 March 2012



AJALI HAINA KINGA

Siku zote watu tunapokuwa wazima huwa tunajisahau sana. Huwa tunadhani wanaostahili kupata ajali ni wengine na sisi hatumo katika orodha hiyo; na wakati mwingine huwa tunafikia hata kukufuru kwa kudhani waliopata ajali walijitakiwa wenyewe ama ni wajinga.

Moja ya maeneo ambayo wengi wetu tumebweteka ni katika vyombo vya usafiri. Laiti kama mungu asingeliingilia kati na kuachia kila uzembe unaofanyika katika vyombo vya usafiri uzae matunda, basi nadhani kufikia leo zaidi ya nusu ya wakazi wa dunia hii wangelikuwa wametoweka kwa ajali.

Utamkuta dareva amejaza abiria kwenye gari lake anakwenda mwendo ambao hata kama itatokezea hitilafu yoyote japo ndogo aidha barabarani ama katika gari lake basi hatakuwa na namna yoyote ya kuokoa maisha ya watu aliowabeba.

Sambamba na madereva, na abiria nao mara nyingi wanachangia kwani ni wepesi wa kuhimiza dareva aende mwendo kasi ili waweze kuwahi waendako ama wakati mwingine ni asili ya ushabiki usio na sababu wa kupenda mwendo mkali.

Zamani tatizo lilikuwa katika magari, lakini sasa hivi kumekuja usafiri wa  pikipiki au bodaboda. Vyombo hivi vimekuwa ni hatarishi kiasi ambacho tunaweza kusema ni janga la Taifa. Jamaa waendeshao vyombo hivi wamekuwa wakorofi barabarani kiasi kwamba maisha yao wamekwisha yakabidhi mbinguni na wao wanatembea  wakiwa kama maiti watembeao. Bodaboda hawajali kama kuna kuanguka ama kugonga, wanachokijua wao ni kufika haraka iwezekanavyo huko waendako.

Abiria wa bodaboda nao sijui ni kwa sababu ya ukata ama vipi, hulazimisha kupanda wengi katika pikipiki moja kana kwamba wako  katika mchezo wa sarakasi. Wengine kama si wanene hupanda watatu na dareva kuwa wane katika pikipiki moja; wenyewe wanaita mishikaki.

Sasa kama tunafanya uzembe wa makusudi kwa kisingizio cha kuwa ajali haina kinga tuendelee mpaka yaje kutukuta na hapo ndipo tutakuja kujua kama ajali ina kinga au haina.


No comments:

Post a Comment