Tunaruhusu watu wachungulie dirishani na kueleza walichokiona. Tunashauri wasiingie ndani kuhofia yatakayowakuta. Tunawaomba waseme ya muhimu kwa jamii na yasiyo muhimu iwe siri yao.
Saturday, 31 March 2012
Friday, 30 March 2012
KAZI USIYOITAKA UNAIOMBA YA NINI ?
Kutokana na hali ilivyokithiri imebidi
niongelee hili pia kwani kwa hakika wengi wetu linatukera.
Jambo hili ni tabia ya baadhi ya watu ambao
wamezagaa katika huduma mbalimbali lakini wana tabia chafu ambazo haziendani
na maadili ya huduma wanazozitoa.
Utamkuta mtu mwanamama au hata baba yuko
hoteli kazi yake ni kuhudumia watu kuwasikiliza
waagizacho na kuwaletea wakitakacho lakini yeye daima ni kufanya ndivyo
sivyo. Utamkuta sijui ni kwa sababu gani, lakini huwa hasikilizi maagizo hadi
mwisho. Mtu ataagiza aletewe wali kwa nyama ya kuku, lakini yeye kama zuzu anamletea ugali kwa samaki. Anapolalamikiwa
kuwa hivyo havikuagizwa, bila ya hata aibu huanza mabishano kwamba yeye ni
mzoefu wa kazi yake na hawezi kukosea na maneno mengi ya kashfa kwa mteja.
Ama utamkuta dada yuko baa kazi yake kuuza
bia. Mteja atafika kwenye baa hiyo, yeye hajali amezama anasoma gazeti la
Ijumaa hujku akicheka pekeyake. Mteja akimstua ampe huduma huinuka huku
akisonya na kwenda kuleta Kilimanjaro baridi kwa mteja bila ya hata kumuuliza
na kumfungulia. Mteja akionyesha kushangaa, mhudumu huyu humbwatukia maneno na
kusisitiza kuwa lazima alipie hicho kinywaji.
Ukienda hospitali nako kuna mengine.
Watuwanakwenda na mgonjwa mahututi wanahangaika kumshusha kwenye gari, wahudumu
na wamekaa wanaongelea kombe la UEFA. Ukiwauliza mbona hawachangamki,
wanakujibu kuwa wao hawashughulikii eneo
hilo wasubiriwe
wanaohusika. Wenye mgonjwa wakitaka kuchukua machela wambebe mgonjwa wao
wanakuja juu na kuwambia hiyo machela ni ya chumba cha maiti wasiiguse. Watu
hubaki wameduwaa hawaelewi wafanye nini; maana hawaelekezwi wafa kufahamishwa
utaratibu ukoje.
Mambo haya ya huduma mbovu yamezagaa kila
kona. Nenda Polisi, nenda mahakamani, nenda sokoni, madukani, mashuleni n.k.
Watu wanafanya kazi kama wamelazimishwa.
Wanafanya kazi kama wanajitolea kumbe
wanalipwa kwa kazi hizo. Sasa jamani ni kwanini watu wanaomba kazi
wasizozipenda na wasio na wito nazo ?
Wednesday, 28 March 2012
GUBU LINAKERA KUPITILIZA
Katika mambo ambayo binadamu wengi hawawezi kuyavumilia; basi ni
gubu.
Mtu mwenye gubu kwa kawaida huwa hana simile, hana subira, hana
shukurani, hana huruma, na nadiriki kusema hata dini hana. Mtu mwenye gubu
hajui kusamehe, hajui kusahau, hajui kubembeleza; yeye daima ni kulaumu,
kulalamika, kusimanga, na kelele kibao. Naweza kusema ni heri ya mkorofi au
mpigaji kuliko mwenye gubu.
Mwenye gubu hana dogo, mwenye gubu haridhiki mwenye gubu daima
mdomo wake uko wazi unamwaga maneno kama bomba
la maji nmachafu.
Mwenye gubu hudhani kuwa yeye ndiye anayejua, yeye ndiye
anayeonewa, yeye ndiye mwangalifu; kwa ujumla mwenye gubu ni mbinafsi. Mwenye
gubu hamwamini mwingine pamoja na kwamba yeye hujion ndiye anaaminika.
Kama hujawahi kuishi na mwenye gubu huwezi kuyajua haya, lakini
kwa wale ambao wamepambana nao wanalijua hili; mwenye gubu ni moto wa kuotea
mbali.
Lakini katika wenye gubu, wapo waliozaliwa na gubu hilo na wapo ambao wanatwezwa na mazingira
au hali ya maisha kwa wakati ule. Pasmoja na tofauti zao hayuko mwenye nafuu.
Niseme tu kuwa gubu linakondesha haraka kushinda hata njaa.
Tuesday, 27 March 2012
NYAMA YA KUKU.
1. Nina swala laniasi, nahitaji msaada,
Limekuwa si rahisi, kwangu imekuwa mada,
Sina hakika nahisi, jibu linanipa shida,
Hasa ni
kiungo gani, kitamu nyama ya kuku.
2. Zinanitoka kamasi, nazidi poteza muda,
Naingiwa wasiwasi, kama nimepanda
boda,
Swali limenisha kasi, nimekwama kama
uda,
Hasa ni
kiungo gani, kitamu nyama ya kuku.
3. Nilidhani filigisi, amenikanusha dada,
Kasema tamu kiasi, ina harufu ziada,
Shomboye kama girisi, mdomoni inakwida,
Hasa ni
kiungo gani, kitamu nyama ya kuku.
4. Paja nikalinakisi, lapendwa hadi
Finida,
Amenipinga Kaisi, amenicheka Sauda,
Eti mimi ndiyo basi, mbumbumbu au labda,
Hasa ni
kiungo gani, kitamu nyama ya kuku.
5. Kuku anao ukwasi, vipande kwake ni
ada,
Ukija kwa kinasisi, wa mitandao ya Voda,
Kidari chashika kasi, lakini si kwa Dauda,
Hasa ni
kiungo gani kitamu nyama ya kuku.
6. Kipapatio wadosi, wasema ndio waheda,
Kinaondoa mikosi, wakila na kuburuda,
Lakini kwa makasisi, hakimo kwenye jalada,
Hasa ni
kiungo gani, kitamu nyama ya kuku.
7 Amenambia Hamisi, kwa shingo ndio
welda,
Akila anajihisi, ameshiba na faida,
Anavua na soksi, na kuimba dadadida,
Hasa ni
kiungo gani, kitamu nyama ya kuku.
8. Makanyagio msosi, wameutaja makada,
Wanywaji kwa magrasi, acha nyinyi wanywa soda,
Kwamba kitu na boksi, kaone kwenye minada,
Hasa ni
kiungo gani, kitamu nyama ya kuku.
9 Ndugu zangu wa Masasi, kabla kuvuka boda,
Ya kichwa wameasisi, wamesifu kina Sada,
Wasema yashinda ngisi, hata uile kwa dida,
Hasa ni
kiungo gani, kitamu nyama ya kuku.
10. Hapa napiga krosi, nisimalize uroda,
Nawaacha waasisi, mnijaze ushuhuda,
Wajue kadamnasi, Kisiju hadi Singida,
Hasa ni
kiungo gani , kitamu nyama ya kuku.
VAZI LA TAIFA
Miongoni
mwa mambo ambayo ni ya msingi kwa Taifa
letu na wananchi wake ni kuwa na utambulisho ambao utamfanya kila mwananchi
wa nchi hii atakapoonekana basi
atambuliwe kuwa ni Mtanzania.
Miongoni
mwa mambo hayo ni vazi la Taifa.
Kumekuwa na
mawazo mengi juu ya vazi gain linalofaa kuwa vazi la Taifa. Mimi nami kama
Mtanzania sina budi kuchangia juu ya suala hili.
Nimekuwa nikiyaona mavazi mengi yanayopendekezwa kuwa
mavazi ya Taifa. Tatizo nililogundua ni kuwa kwa kiasi Fulani tumekuwa nyuma
kiubunifu kiasi kwamba mavazi au mitindo mingi inayoonyeshwa au kupendekezwa ni
kama tunairudia au kuiiga toka kwa mataifa
mengine.
Mimi kwa maoni yangu ningelipenda sisi tujikite katika
rangi nne kwanza za taifa ambazo ni kijani; kwamba mtu awe huru kushona mtibndo
wowote autakao, lakini pindi utakapokuwa umepangilia rangi zetu zote nne za
taifa yaani kijani, njano, bluu na nyeusi basi vazi hilo liwe tayari ni la taifa.

Pendekezo
langu la pili ni kutumia mavazi ya kimasai lakini katika rangi za taifa, basi hilo nalo liwe vazi la
Taifa. Nasema hivi si kwamba ninadharau mavazi ya makabila mengine, lakini
tutake tusitake, wamasai ndilo kabila pekee ambalo likekuwa na msimamo wa
kulinda vazi lao kila waendako na kila waliko bila ya kuyumbishwa na mavazi
haya ambayo yamekuwa yakiingia nchini mwetu kila siku. Hivyo Taifa kwa
kuwaenzi, ichukue mavazi yao na kuyafanya ni ya Taifa.
MPENZI SHAIRI
Nilikuwa sijasema, siri ya moyoni
mwangu,
Ila leo najituma, kutoa ukweli wangu,
Japo moyo waniuma, hiyo si hiari yangu,
Pokea ukweli wangu, Shairi ninakupenda.
Subscribe to:
Posts (Atom)









